Na Wellu Mtaki, Geita
WAFANYABIASHARA wadogo na wajasiriamali wanaoanza shughuli za biashara kwa mara ya kwanza wametakiwa kuchangamkia fursa ya msamaha wa kodi wa kipindi cha miezi 12, unaodaiwa kutolewa kwa mujibu wa mabadiliko ya sheria za kodi yaliyoanza kutekelezwa Julai 1, 2026.
Rai hiyo imetolewa na Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Justine Katiti, wakati akitoa elimu kwa wananchi katika Maonesho ya Tisa ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Katiti amesema fursa hiyo inalenga kuwapa nafasi wafanyabiashara wanaoanza shughuli zao kujenga na kuimarisha biashara kabla ya kukabiliwa na mzigo mkubwa wa gharama katika hatua za awali.
Amesema wafanyabiashara binafsi wanaoanza biashara kwa mara ya kwanza wanapaswa kufika katika ofisi za TRA kupata elimu na kufahamu taratibu pamoja na vigezo vinavyohitajika ili kunufaika na fursa hiyo.
“Wafanyabiashara wanaoanza biashara kwa mara ya kwanza wanapaswa kufika TRA kupata elimu na kufanya taratibu zinazohitajika ili waweze kuelewa vizuri fursa hii,” amesema Katiti.
Ameongeza kuwa vijana na wajasiriamali wengine hawapaswi kuwa na hofu ya kufika TRA, bali wanapaswa kutumia fursa hiyo kupata elimu sahihi kuhusu sheria za kodi na huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo.
Baadhi ya wafanyabiashara waliopata elimu hiyo katika maonesho hayo wameeleza kuwa taarifa hiyo imewasaidia kuondoa hofu waliokuwa nayo kuhusu masuala ya kodi.
amesema amefurahishwa kupata elimu kuhusu msamaha huo, akieleza kuwa utampa nafasi ya kuendelea kuijenga biashara yake katika hatua za mwanzo.
“Nilipata elimu kuhusu msamaha wa miezi 12 kwa mfanyabiashara anayeanza. Nimefurahi kupata msamaha huo kwa sababu utanisaidia kuendelea na biashara yangu,” amesema.
Amesema awali alikuwa na hofu ya kufika TRA kutokana na dhana kwamba angekabiliwa na gharama kubwa au taratibu ambazo zingeweza kuwa ngumu kwake.
Hata hivyo, amesema elimu aliyopata imemsaidia kubadili mtazamo huo na kuelewa umuhimu wa kufika TRA kupata taarifa sahihi.
“Nitawasihi wafanyabiashara wenzangu wadogo nao waje kupata elimu. Huu msamaha wa miezi 12 utatusaidia sana,” amesema.
Kwa upande wake, mfanyabiashara mwingine, Elisha, amesema elimu hiyo imemsaidia kuelewa namna unafuu huo unavyoweza kumsaidia katika hatua za mwanzo za biashara.
Amesema bado yupo katika hatua ya kujijenga kiuchumi, hivyo fursa hiyo inaweza kumpa nafasi ya kuimarisha biashara yake kabla ya kufikia hatua nyingine za ukuaji.
“Nimepewa mafunzo kuhusu msamaha. Kwa mtazamo wangu, msamaha huu unaweza kunisaidia kwa sababu kwa sasa bado najiimarisha. Ninaamini kadri muda unavyokwenda nitakuwa vizuri,” amesema.
Wafanyabiashara hao wamewahimiza wenzao, hasa wale ambao wamekuwa na hofu ya kufika TRA, kutumia fursa zinazopatikana katika maonesho na ofisi za TRA kupata elimu sahihi kuhusu kodi badala ya kutegemea taarifa zisizo rasmi.
Maonesho ya Tisa ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanaendelea mkoani Geita, yakishirikisha taasisi mbalimbali za Serikali, kampuni, wafanyabiashara na wadau kutoka sekta tofauti.


Comments
Post a Comment