NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray, ametoa maelekezo sita kwa waajiri, watumishi pamoja na Mamlaka za Ajira na Nidhamu, akitaka changamoto za kiutumishi kushughulikiwa kwa wakati ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Qwaray ametoa maelekezo hayo leo wakati wa kikao kazi cha kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara.
Amesema waajiri wanapaswa kuhakikisha stahiki za watumishi, ikiwemo kupandishwa vyeo, uhamisho, malimbikizo ya mishahara na mafao, zinashughulikiwa kwa wakati.
Pia, amewataka waajiri kuhakikisha madai ya watumishi yanahakikiwa ipasavyo na kuwasilishwa yakiwa na nyaraka zote muhimu ili kuwezesha malipo kufanyika kwa wakati.
Katika agizo jingine, amezitaka Mamlaka za Ajira na Nidhamu kusimamia haki na wajibu wa watumishi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma, huku akisisitiza kuachana na utendaji wa mazoea.
Mhe. Qwaray amesema mambo yaliyo ndani ya uwezo wa waajiri na Mamlaka za Ajira na Nidhamu yanapaswa kushughulikiwa katika ngazi hizo badala ya kuendelea kuwasilishwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Aidha, amewataka waajiri kuzingatia mahitaji na tofauti za makundi mbalimbali ya jamii bila ubaguzi, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kujenga Utumishi wa Umma jumuishi na wenye usawa.
Kuhusu maadili, amewataka watumishi kuyafahamu na kuyatekeleza kwa kuzingatia Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma, huku akisisitiza kuwa watumishi wanaokiuka maadili au kutotekeleza majukumu yao ipasavyo wanapaswa kuchukuliwa hatua stahiki za kinidhamu kwa wakati.
Ametaja misingi muhimu ya utumishi kuwa ni kutoa huduma bora, utii kwa Serikali, bidii ya kazi, kutoa huduma bila upendeleo, kufanya kazi kwa uadilifu, kuwajibika kwa umma, kuheshimu sheria na kutumia kwa usahihi taarifa za Serikali.




Comments
Post a Comment