Silaha ya Wachimbaji Matumizi ya takwimu rasmi yanapaswa kuwa sehemu ya msingi katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya taifa, ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja Takwimu Mkoa wa Geita, Khalid Msabaha wakati taasisi hiyo ikishiriki katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.
Msabaha amesema ili kufikia malengo ya muda mrefu ya maendeleo, ni muhimu kwa serikali, wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wengine kutumia takwimu rasmi katika kupanga na kufanya maamuzi.
Katika muktadha wa Geita, ambako shughuli za madini ni sehemu muhimu ya uchumi wa eneo hilo, matumizi ya takwimu yana umuhimu katika kuelewa siyo tu kiwango cha uzalishaji, bali pia shughuli zinazozunguka sekta hiyo.
Hii inahusisha mnyororo mpana wa thamani unaogusa biashara, huduma, usafirishaji, ajira na shughuli nyingine za kiuchumi zinazochochewa na sekta ya madini.
Kwa mujibu wa Msabaha, takwimu siyo namba zinazokusanywa kwa ajili ya kumbukumbu pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kuelewa mwenendo wa uchumi, kupanga shughuli za uzalishaji na kufanya maamuzi yanayozingatia uhalisia wa kiuchumi.
Msabaha ameeleza kuwa sekta ya madini imeendelea kuwa miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi wa Tanzania, huku takwimu zikionyesha kuwa shughuli za uchimbaji wa madini zilichangia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa mwaka 2025.
Sambamba na hilo, amesema kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania imefikia asilimia 6.1 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, ikilinganishwa na asilimia 5.9 mwaka 2025.
Msabaha amesema takwimu hizo zinaonyesha umuhimu wa kuendelea kuwa na taarifa sahihi na zinazopatikana kwa wakati ili kusaidia wadau wa sekta mbalimbali kuelewa mwenendo wa uchumi na kupanga shughuli zao.
Aidha, amesema uwepo wa taasisi hiyo kwenye maonyesho hayo unalenga kuwaelimisha wadau kuhusu umuhimu wa kutumia takwimu rasmi katika kufanya maamuzi ya kiuchumi, hususan katika sekta ya madini na mnyororo wake wa thamani.
Taarifa hiyo imetolewa Septemba 30,2026 na Meneja Takwimu Mkoa wa Geita, Khalid Msabaha wakati taasisi hiyo ikishiriki katika Maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha matumizi ya takwimu rasmi katika shughuli za kiuchumi.
Ushiriki wa NBS katika Maonyesho ya Teknolojia ya Madini Geita unaipa taasisi hiyo nafasi ya kuwafikia moja kwa moja wadau wa sekta hiyo na kuwaeleza umuhimu wa takwimu katika shughuli zao.
Kwa mtazamo huo, takwimu zinakuwa kiungo kati ya hali halisi ya uchumi na maamuzi yanayochukuliwa kuhusu uzalishaji, uwekezaji na maendeleo.
Kupitia maonyesho hayo, NBS inalenga kuongeza uelewa kuhusu upatikanaji na matumizi ya takwimu rasmi, huku ikiendelea kusisitiza kwamba maamuzi yenye tija yanahitaji taarifa sahihi, zinazopimika na zinazoaminika.
Kwa Tanzania inayolenga kuongeza uzalishaji na kuimarisha sekta zinazochangia ukuaji wa uchumi, ujumbe wa NBS ni kwamba takwimu hazipaswi kubaki kwenye ripoti pekee.
Mwisho


Comments
Post a Comment