Na Mashaka Mhando, Iringa
UJENZI wa kituo cha kisasa cha utalii mkoani Iringa, kinachotarajiwa kuwa mkombozi na kiungo muhimu cha kukuza utalii katika Ukanda wa Kusini, umefikia asilimia 88 na unatarajiwa kukamilika rasmi ifikapo Desemba mwaka huu.
Kituo hicho cha kimkakati kimejengwa kikiwa na huduma zote za kisasa, ikiwemo ngazi za umeme (escalators), kumbi za mikutano, pamoja na ofisi zitakazowakutanisha wadau wote wa sekta ya utalii chini ya jengo moja.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, ameeleza kuridhishwa kwake na kasi pamoja na ubora wa kazi inayofanyika alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo leo, Septemba 30, 2026.
Miradi Mingine na Mkakati wa Ukanda wa Kusini
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Dkt. Abbasi alibainisha kuwa kukamilika kwa kituo hicho ni muendelezo wa juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya utalii kusini mwa Tanzania, ikitanguliwa na kukamilika kwa jengo la utafiti mkoani humo.
“Ujio wa jengo hili unafuatia pia kukamilika kwa jengo jingine la masuala ya utafiti. Na jana tumeona uwanja wa ndege wa Mikumi ukimaliziwa, lakini pia Iringa kule Ruaha viwanja viwili vya ndege, majengo ya wageni (hostels), na majengo mengine pia vilishakamilika,” alisema Dkt. Abbasi.
Aliongeza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mingine ya kimkakati katika Hifadhi za Kitulo na Katavi ili kuhakikisha fursa za kitalii katika Ukanda wa Kusini zinatumika kikamilifu.
“Kwa ufupi, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu mpendwa Dkt Samia Suluhu Hassan, ipo kazini katika kuendeleza na kukuza utalii Ukanda wa Kusini,” alisisitiza Katibu Mkuu huyo.







Comments
Post a Comment