Na Mwandishi wetu Jovina Massano.
Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Musoma (MUWASA) Mkoani Mara yawaomba radhi wateja wake kutokana na hitilafu ya mitambo ya kusukuma maji iliyopo kwenye chanzo Cha maji Bukanga hali iliyopelekea upatikanaji hafifu wa maji katika baadhi ya maeneo.
Hayo yameelezwa na kaimu mkuu wa kitengo cha mawasiliano na uhusiano kwa Umma Chausiku Joseph mara baada ya kupokea taarifa ya malalamiko ya wateja wa maji wa maeneo ya Buhare,Rwamlimi,Mtakuja,Kwangwa,Kigera,Songe,majengo,Kariakoo,Zanziba,na Kijiji cha Nyabange.
Chausiku amesema kuwa Mamlaka inaendelea kufanya jitihada kubwa kuhakikisha huduma inajerea kupitia wataalam ambao wanaendelea kufanya marekebisho na maboresho ya mitambo hiyo.
Ameongeza kuwa hivi sasa timu ya wataalam wa MUWASA inaendelea na ufuatiliaji katika maeneo mbalimbali ili kuweza kuimarisha huduma kwa wateja.
"Ndani ya siku kadhaa zilizopita kulikuwa na changamoto ya huduma ya maji kutokana na hitilafu ya mitambo ya kusukuma maji siku ya tarehe 13,8,2023 taarifa imetolewa ya maboresho na tayari huduma imeanza kupatikana na tunaomba wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kwa kuwa wataalam wanaendelea kurekebisha mitambo, amesema Chausiku.
Amewaomba wananchi ambao wanakumbwa na kadhia hiyo kutoa taarifa kwa Mamlaka kwa kuwa ipo tayari kuwahudumia wananchi kupitia namba huku 0800110108 akiwasisitiza wananchi kutoa ushirikiano wa uharibifu miundombinu na kutoihujumu.
Maeneo yanayoathirika zaidi ni yaliyopo pembezoni mwa mji kutokana na kuwepo kwa muinuko endapo hitilafu ikitokea ya mitambo au umeme maeneo hayo mzunguko huharibika na ujazo hupungua kutoka mita 36 hadi kufikia mita za ujazo 22 ambapo mita zinakuwa zimepungua na kuchangia adha hiyo kwa wateja.
Kawaida maji yanatakiwa kuwepo muda wote yasukumwe mfululizo ikitokea hitilafu ya mitambo au umeme athari hutokea.
Kwa Upande wao wateja waliopo katika maeneo hayo wamedai kuwa hawapati taarifa yeyote kutoka kwa Mamlaka hali ambayo inawapa wakati mgumu wa huduma ya maji.
Aidha wateja wamesema huduma ya maji imekuwa ikirejea majira ya saa 8 usiku wakati muda huo wanakuwa tayari wamelala na alfajiri saa 11 huduma hiyo hukoma hivyo wameiomba Mamlaka kutoa taarifa kwa wakati ili wateja waweze kupata maji kwa uhai wao kwa kuwa maji ni uhai.
Wamesema kuwa msemo wa kumtua mama ndoo kichwani unakuwa ni kitendawili kwani hali hiyo imeanza kuwa endelevu na kupelekea wasiwasi wa huduma.
Mbali na changamoto hiyo pia wamelalamikia malipo makubwa ya ankra ya maji kwa madai kuwa haiendani na matumizi husika.
Chausiku ametolea ufafanuzi kuwa Mamlaka haina lengo la kutoa maji usiku na kuhusu ankra ya maji hulipiwa kulingana na matumizi ya mteja mwenyewe ambayo yanakuwa yamehesabika kupitia mita ya mteja huyo.
Amemalizia kwa kuomba ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi ili kuhakikisha kila mtu amepata huduma ya maji ipasavyo.
Je Wizara ya maji kupitia waziri wake ana yapi kwa wakazi wa Manispaa ya Musoma kuhakikisha huduma inarejea kama hapo awali?








Comments
Post a Comment