Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mhe. Mary Daniel Surati, amewahimiza wanafunzi kuendelea kusoma kwa bidii, kuweka malengo makubwa na kutumia fursa za elimu kujijengea msingi imara wa maisha na maendeleo ya jamii.
Mhe. Surati ameyasema hayo aliposhiriki Usiku wa Tuzo kwa Wadau wa Elimu uliofanyika katika Shule ya Sekondari Manga wilayani Tarime, ambapo hafla hiyo iliambatana na utoaji wa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo.
Hafla hiyo imekuwa sehemu ya kutambua na kuenzi juhudi za wanafunzi walioonesha umahiri katika masomo, huku ikiwahamasisha wengine kuongeza bidii ili kufikia mafanikio makubwa zaidi kitaaluma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Surati amesema amefurahishwa na jitihada zinazofanywa na wanafunzi, walimu, wazazi pamoja na wadau mbalimbali wa elimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira yanayowawezesha kufanya vizuri na kutimiza ndoto zao.
Amesema mafanikio ya mwanafunzi hayajengwi na juhudi za mtu mmoja pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya mwanafunzi, mwalimu, mzazi na jamii kwa ujumla.
Katika kuendelea kuhamasisha wanafunzi kufanya vizuri, Mh. Surati alitoa ahadi ya kumpeleka Bungeni mwanafunzi aliyefanya vizuri katika Mtihani wa Kidato cha Sita na kupata Division I ya Alama 4 (1.4), ili apate fursa ya kujifunza na kuona kwa vitendo namna shughuli za Bunge zinavyotekelezwa.
Kwa mujibu wa Mhe. Surati, fursa hiyo inalenga kuwa kichocheo cha kuongeza hamasa kwa mwanafunzi huyo na wanafunzi wengine, kwa kuwaonesha kuwa juhudi, nidhamu na kujituma katika masomo vinaweza kufungua milango ya fursa mbalimbali.
Amesema ni muhimu wanafunzi kujifunza kuwa mafanikio huanza kwa kuweka malengo, kufanya kazi kwa bidii na kuwa na nidhamu katika kufuatilia ndoto zao.
“Ninaamini hatua hii itakuwa motisha kwake na kwa wanafunzi wengine kuendelea kusoma kwa bidii, kuweka malengo makubwa na kuamini katika uwezo wao,” amesema Mh. Surati.
Aidha, amewapongeza wanafunzi wote waliofanya vizuri na kuwataka wasitosheke na mafanikio waliyoyapata, bali waendelee kujitahidi zaidi ili kufikia viwango vya juu katika elimu na taaluma zao.
Vilevile, amewapongeza walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwaandaa wanafunzi kitaaluma na kimaadili, huku akiwashukuru wazazi na wadau wa elimu kwa mchango wao katika kuimarisha sekta hiyo.
Amesema uwekezaji katika elimu ni uwekezaji wa muda mrefu unaolenga kuandaa vijana wenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.
Mhe. Surati amesisitiza kuwa hafla kama hiyo ni muhimu kwa sababu, mbali na kutambua juhudi za wanafunzi waliofanya vizuri, pia inajenga utamaduni wa kuthamini elimu na kuhamasisha ushindani wenye tija miongoni mwa wanafunzi.
Amewataka wanafunzi waliopokea tuzo kuzitumia kama chachu ya kufanya vizuri zaidi, huku wale ambao hawakupata tuzo wakihimizwa kutokata tamaa, bali kuongeza bidii na kujifunza kutokana na mafanikio ya wenzao.
Ameeleza kuwa mafanikio ya wanafunzi ni fahari kwa wazazi, walimu na jamii nzima, hivyo kila mdau ana wajibu wa kuendelea kuweka mazingira bora yatakayowawezesha vijana kutimiza ndoto zao.
“Hongereni sana wanafunzi wote waliofanya vizuri. Endeleeni kusoma kwa bidii, kuweka malengo makubwa na kuamini katika uwezo wenu. Elimu ni msingi wa mafanikio na maendeleo ya jamii yetu,” amesema Mh. Surati.





Comments
Post a Comment