Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Mwigulu Nchemba, amesema Serikali imeanza kuchukua hatua za kuondoa vitendo vinavyowakwamisha wananchi kufanya shughuli za uzalishaji na biashara, huku ikielekeza nguvu katika kuboresha elimu, kutatua migogoro ya ardhi na kuhakikisha fedha za maendeleo zinatumika kwa uadilifu.
Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Sokoine, wilayani Serengeti, mkoani Mara, leo Jumatano, Julai 1, 2026.
Amesema Serikali haitaki kuona wafanyabiashara na wananchi wanaofanya kazi kwa halali wakinyanyaswa kwa kukamatwa mali zao bila sababu za msingi, ikiwemo kufungiwa akaunti za benki, kuchukuliwa fedha, pikipiki, baiskeli na vifaa vyao vya kazi.
Katika sekta ya usafiri,Dkt. Nchrmba amesisitiza kuwa Serikali imeelekeza vyombo vya dola kutokamata pikipiki na magari yanayotumika halali kama mitaji ya wananchi isipokuwa pale ambapo vyombo hivyo vitahusishwa moja kwa moja na uhalifu mkubwa usio na dhamana, ikiwemo biashara ya dawa za kulevya, usafirishaji wa nyara za Serikali au makosa mengine makubwa ya jinai.
Pia amewataka askari wanaowasimamia waendesha bodaboda kutumia busara wanapotekeleza sheria ili kulinda maisha ya wananchi, akisisitiza kuwa Serikali haitaki kuona vijana wakipoteza maisha kutokana na ukimbizaji usio wa lazima.
Waziri Mkuu pia ameonya vikali watumishi wanaohujumu fedha za miradi ya maendeleo, akisema Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kutumia vibaya fedha za wananchi.
Amesema amepokea taarifa mbalimbali kuhusu utekelezaji wa miradi mkoani Mara na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kufanya ubadhirifu.
Kuhusu migogoro ya ardhi,Dkt. Nchemba amesema Serikali imeanza kusafisha mfumo huo baada ya kubaini baadhi ya watumishi wanaotumia nafasi zao kuzalisha migogoro kwa maslahi binafsi.
Ameeleza kuwa Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaandaa mfumo wa kudumu utakaosaidia kupunguza migogoro hiyo na kuhakikisha haki inapatikana kwa wananchi.
Amesema Serikali imezipokea hoja zote zilizowasilishwa na wananchi wa Serengeti na kuwaagiza mawaziri walioambatana naye kuzifanyia kazi kwa kila sekta ili kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.








Comments
Post a Comment