Mbunge wa Rorya, Jafari Chege, ameiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mamlaka ya Mji Mdogo Shirati, akieleza kuwa wananchi bado wanakabiliwa na changamoto za maji, umeme, barabara na ukosefu wa soko la kisasa.
Akizungumzia huduma ya maji, Chege amesema licha ya uwekezaji uliofanyika, wananchi wengi wa Shirati bado hawapati maji safi na salama kwa uhakika.
Amesema akina mama na wananchi wengine wanaendelea kutumia muda mwingi kutafuta maji, hivyo kuiomba Serikali kueleza changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa huduma hiyo na kuhakikisha mradi wa maji unakamilika ili wananchi wanufaike.
Kuhusu umeme, amesema huduma hiyo ni muhimu katika kukuza biashara, viwanda vidogo na shughuli nyingine za kiuchumi, hivyo ameomba Serikali kuendelea kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika ili kuongeza kasi ya maendeleo katika eneo hilo.
Aidha, Mbunge huyo ameomba Serikali kuharakisha ujenzi wa barabara za lami zilizoahidiwa, akisema miundombinu hiyo itarahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, kuongeza fursa za biashara na kuinua uchumi wa wananchi wa Shirati na Wilaya ya Rorya kwa ujumla.
Chege pia ameiomba Serikali kujenga soko la kisasa katika Mamlaka ya Mji Mdogo Shirati, akieleza kuwa soko hilo litawawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika mazingira bora, kuongeza mapato ya wananchi na kuifanya Shirati kuwa kitovu cha biashara katika ukanda huo.
Mbunge Chege amesisitiza kuwa maendeleo yote hayo yatafanikiwa ikiwa amani na utulivu vitaendelea kudumishwa nchini. Amewataka wananchi kuendelea kuilinda na kuitunza amani ya Tanzania, akieleza kuwa ndiyo msingi wa maendeleo, uwekezaji na utekelezaji wa miradi yote ya Serikali.







Comments
Post a Comment