AGNES MARWA AIOMBA SERIKALI KUHARAKISHA MIKOPO YA VIZIMBA, AKAZIA BANDARI YA KIRONGWE NA BARABARA YA RORYA
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Mhe. Agnes Marwa, amemwomba Waziri Mkuu kuagiza kutolewa kwa haraka mikopo ya programu ya VIZIMBA kwa vikundi vinane vya Wilaya ya Rorya vilivyokamilisha taratibu zote za kupata fedha hizo, akisema hatua hiyo itawawezesha wananchi kujiajiri, kuongeza uzalishaji na kupunguza umaskini.
Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Rorya, Mhe. Marwa amesema vikundi hivyo vimekidhi vigezo vinavyohitajika, hivyo vinasubiri tu fedha ziweze kutolewa ili vianze kutekeleza shughuli za maendeleo na kuinua uchumi wa wananchi.
Mbali na suala la mikopo, Mhe. Marwa ameiomba Serikali kuharakisha uboreshaji wa Bandari ya Kirongwe, akieleza kuwa Rorya ni wilaya inayopakana na Kenya, hivyo bandari hiyo ina nafasi muhimu katika kukuza biashara za mipakani, kuongeza fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa eneo hilo.
Aidha, amemshukuru Rais Samia na Serikali kwa kuendelea kupeleka fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani Rorya, ikiwemo ukarabati wa barabara ambao umeanza kuleta nafuu kwa wananchi. Hata hivyo, amesisitiza haja ya kukamilisha sehemu zilizobaki za barabara hiyo ili iwe katika kiwango bora na iweze kutumika kwa urahisi katika misimu yote ya mwaka.
Mhe. Marwa amesema barabara hiyo ni mhimili mkubwa wa shughuli za kiuchumi katika Wilaya ya Rorya, hivyo kukamilika kwake kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa, huduma za kijamii na mawasiliano kati ya wananchi.
Mbunge huyo alimkaribisha Waziri Mkuu wilayani Rorya na kumtakia afya njema na hekima katika kuendelea kuwatumikia Watanzania na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.




Comments
Post a Comment