Mchimbaji mdogo wa madini kutoka Geita, Tuguro Zakayo, ameiomba Serikali kuimarisha utaratibu wa utatuzi wa migogoro ya maeneo ya uchimbaji ili kulinda mitaji na uwekezaji wa wachimbaji wadogo nchini.Akizungumza Leo Septemba 28,2026 aliposhiriki siku ya Mabenki Kwenye Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolokia ya Madini yanayofanyika Katika Viwanja vya Dkt Samia Suluhu Hassan Mkoani Geita Zakayo amesema changamoto kubwa inayowakabili wachimbaji wadogo ni ukosefu wa mtaji pamoja na migogoro ya maeneo ya uchimbaji, hali ambayo imekuwa ikisababisha baadhi yao kupata hasara kubwa baada ya kuwekeza fedha na kuanza shughuli za uchimbaji.
Amesema katika moja ya maeneo waliyokuwa wakifanya shughuli za uchimbaji, walitumia kipindi cha mwaka mmoja na miezi mitano huku wakiwekeza zaidi ya shilingi milioni 230.
Kwa mujibu wa Zakayo, baada ya kufanya uwekezaji huo na kuendelea na shughuli za uchimbaji, waliondolewa katika eneo hilo kwa madai kwamba wamevamia eneo ambalo linamilikiwa kwa leseni na mtu mwingine.
Amesema hali hiyo imewaweka katika mazingira magumu kutokana na kuwa walikuwa wakilipa mrabaha wa Serikali na kufuata taratibu zote halali, ikiwemo kuwa na kumbukumbu kwenye vitabu vya Serikali.
“Changamoto kubwa ya kwanza ni mtaji. Changamoto nyingine ni maeneo ya uchimbaji. Unavumbua eneo jipya na kuanza kuchimba, lakini baadaye anatokea mtu anayedai kuwa ana leseni ya eneo hilo na anakuondoa,” amesema Zakayo.
Amesema kutokana na mgogoro huo, shughuli za uchimbaji katika eneo hilo zimesimama tangu mwezi wa kwanza mwaka huu, huku wakisubiri ufafanuzi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Zakayo amesema hali hiyo imekuwa ikiwatia hasara wachimbaji wadogo ambao huwekeza fedha nyingi katika utafiti, uchorongaji na shughuli nyingine za maandalizi kabla ya kuanza kupata matokeo ya uwekezaji wao.
Ameiomba Serikali kuingilia kati changamoto hiyo na kuweka utaratibu mzuri wa kutatua migogoro ya leseni na maeneo ya uchimbaji, ili kuhakikisha wachimbaji wadogo wanakuwa na uhakika wa maeneo wanayofanyia shughuli zao na kulinda uwekezaji wao.
Amesema utaratibu huo utasaidia kupunguza migogoro kati ya wachimbaji wadogo na wenye leseni, pamoja na kuwapa wachimbaji uhakika wanapowekeza mitaji yao katika shughuli za uchimbaji wa madini
Comments
Post a Comment