Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limejitokeza kwa kishindo katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita, kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali kuhusu fursa na teknolojia zinazotumika katika sekta ya mafuta na gesi nchini.
Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Masoko wa TPDC, Grace Chigugu, amesema ushiriki wa TPDC unalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu majukumu ya shirika hilo, pamoja na fursa zinazopatikana katika sekta ya mafuta na gesi asilia.
Grace amesema TPDC inatekeleza majukumu yake ya kimkakati kuanzia katika utafiti na utafutaji wa mafuta na gesi, uzalishaji, uchakataji hadi usambazaji wa nishati hiyo kwa matumizi mbalimbali.
Ameeleza kuwa katika maonesho hayo, wataalamu wa TPDC wanatoa elimu kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa zinazosaidia katika utambuzi wa miamba yenye viashiria vya mafuta na gesi, pamoja na mifumo ya kisasa ya uchorongaji na usafirishaji.
Aidha, Grace amesema wananchi wanaotembelea banda la TPDC wanapata fursa ya kujionea teknolojia ya Ukweli Uhalisia (Virtual Reality - VR), inayowawezesha kushuhudia kwa karibu namna miradi mikubwa ya uchorongaji na usafirishaji wa gesi asilia inavyotekelezwa.
“Kupitia teknolojia hii ya Virtual Reality, wananchi wanapata fursa ya kujifunza na kuona kwa karibu namna shughuli mbalimbali za mafuta na gesi zinavyotekelezwa, bila kulazimika kwenda katika maeneo ambayo miradi hiyo inafanyika,” amesema Grace.
Ameongeza kuwa ushiriki wa TPDC katika maonesho hayo ni sehemu ya jitihada za kuendelea kuwafikia wananchi na kuwapa uelewa kuhusu sekta ya mafuta na gesi, pamoja na fursa za uwekezaji na huduma zinazotolewa na shirika hilo.
Kwa upande wa Mkoa wa Geita, Grace amesema mkoa huo unaendelea kunufaika na miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali kupitia TPDC, ikiwemo Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ambalo linapita katika maeneo mbalimbali na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Amesema pia kupitia kampuni yake tanzu ya TANIL (Tanoil), TPDC inamiliki na kuendesha kituo cha mafuta mkoani Geita, kinachotoa huduma za nishati kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo usafirishaji na shughuli zinazohusiana na sekta ya madini.
Akizungumzia mipango ya baadaye, Grace amesema Serikali inaendelea na mipango ya kupeleka na kusambaza gesi asilia katika mikoa ya kanda ya kaskazini na kati, ikiwemo Morogoro, Dodoma, Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
Amesema mipango hiyo pia inalenga kuhakikisha miundombinu ya gesi asilia inaendelea kupanuka na kufikia maeneo mengine, ikiwemo Mkoa wa Geita, katika miaka ijayo.
“Lengo ni kuhakikisha wananchi na viwanda vinapata nishati ya uhakika na kwa gharama nafuu, sambamba na kuchochea shughuli za uzalishaji na uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema Grace.
TPDC imeendelea kuwataka wananchi, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini kutembelea banda lake katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Geita ili kupata elimu zaidi kuhusu shughuli za shirika hilo, teknolojia zinazotumika katika sekta ya mafuta na gesi, pamoja na fursa za uwekezaji na huduma zinazotolewa.

Comments
Post a Comment