Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) leo Septemba 28, 2026, imetunukiwa tuzo ya mshindi wa pili katika kundi la Taasisi za Umma zisizo za Kibiashara zinazofanya vizuri katika usimamizi na matumizi bora ya fedha (Best Financial Management Performance – Non-Commercial Entities).
Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo A. Saqware, na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, katika Kikao cha Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Umma (CEOs Forum) kinachoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), jijini Arusha.
Tuzo hizo zimeandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa lengo la kutambua Taasisi za Umma zinazofanya vizuri katika maeneo mbalimbali ya usimamizi na matumizi ya rasilimali za umma. Akieleza kuhusu kundi la Matumizi Bora ya Fedha, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, amesema tathmini hiyo imezingatia ufanisi katika matumizi na ukusanyaji wa mapato, pamoja na hatua za kupunguza utegemezi kwa Taasisi za Umma zisizo za Kibiashara.
Ameeleza zaidi kuwa Taasisi zilizofanya vizuri katika kundi hilo zimeonesha kuimarika kwa mapato, udhibiti wa matumizi, kupungua kwa utegemezi, pamoja na kuboreka kwa upatikanaji wa ziada na ukwasi, kwa kuzingatia taarifa za hesabu zilizokaguliwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
TIRA, Kwa Soko Salama la Bima



Comments
Post a Comment