Na Mwandishi wetu Jovina Massano Musoma.
Baadhi ya Wananchi mkoani Mara waupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii(NSSF) kwa kuwafikia na kuwapa elimu ya kina kuhusu umuhimu wa mfuko huo.
Wamesema elimu inayotolewa hivi sasa imewasaidia kuelewa umuhimu wa kujiwekea akiba na fursa zilizopo katika mfuko huo.
Hivi sasa timu ya maafisa maelekezo ya hifadhi skimu ikiongozwa na Athanas Lukuba pamoja na Philipo Kachinde inaendelea kutoa elimu sambamba na kusajili wanachama kutoka makundi mbalimbali katika wilaya zilizopo mkoani Mara.
Mpaka sasa NSSF imewafikia Wajasiriamali na vikundi mbalimbali wakiwemo wachimbaji wadogo na kuwaelimisha kuhusu Hifadhi ya Jamii.
Salome Maganga Nyaluga mkazi wa Mtaa wa Majita road ameipongeza NSSF kwa kuwafikia na kuwapa elimu ya kutosha na kupata uelewa juu ya mafao yaliyopo hasa upande wa matibabu ambayo yamelatibiwa na Wizara ya afya.
"Maamuzi ya mfuko huu kufika katika mitaa na kuelimisha Wananchi ni jambo zuri kwa kuwa Wajasiriamali wengi hajui kama NSSF ni kwa ajili ya watu ambao hawajaajiriwa na Serikali", amesema Salome.
Kwa Upande wao Samson Nzunguni mkazi wa mtaa wa VETA na Alexandra Kilugu wamewashukuru na kuwapongeza maafisa hao kwa ufafanuzi na majibu mazuri yaliyoweza kuwapa ufahamu wa kutosha juu ya huduma za NSSF.
Septemba 14 ,2026 timu hiyo ya NSSF imefanikiwa kufika wilayani Bunda na kuweza kuwafikia Wananchi waliopo vijijini wakiwemo wachimbaji madini wadogo zoezi limefanyika ndani ya wiki moja ndani ya wilaya hiyo ambapo walipata ushirikiano kutoka kwa viongozi wa maeneo hayo.
Wananchi na wachimbaji madini wadogo hao mara baada ya kupata elimu ya kutosha wameweza kuhamasika na kuchukua maamuzi ya kujiunga na NSSF.
Maafisa hao wamefafanua sifa za kujiunga na NSSF na Kujiandikisha katika Skimu hii,mwanachama anapaswa awe na umri wa kuanzia miaka 15 hadi 70 na asiwe ni mnufaika wa mafao ya Pensheni kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini.
Mbali na sifa hizo pia anatakiwa kuwa Mtanzania na mkazi wa Tanzania Bara ili aweze kujiunga na kujiandikisha katika Skimu hii,mwanachama anapaswa kujaza fomu ya uandikishaji kwa kuweka taarifa binafsi.
Taarifa hizo ambazo ni namba ya kitambulisho cha Taifa (NIDA) au Leseni ya udereva au kitambulisho cha mpiga kura pia anaweza kuwasilisha fomu kwa njia ya mtandao au kufika kwenye ofisi za Mfuko katika mkoa alipo.
Kampeni hii ni endelevu na yenye manufaa kwa jamii kwa mustakabari wa maendeleo na uchumi wa Wananchi na Taifa.












Comments
Post a Comment