Benki ya NMB imeweka utaratibu unaowawezesha wachimbaji wadogo kutumia vifaa vya uchimbaji kama dhamana ya kupata mkopo, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya dhamana inayowakabili wachimbaji wengi.
Akizungumza katika Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, Mkuu wa Idara ya Biashara NMB, Deogratias Shirima, amesema kupitia utaratibu huo mchimbaji anaweza kupata kati ya asilimia 50 hadi 80 ya thamani ya vifaa anavyohitaji kulingana na tathmini na vigezo vya benki.
Amesema jumla ya zaidi ya Sh bilioni 350 zimetolewa na benki hiyo hadi kufikia Julai mwaka huu kwa ajili ya shughuli zinazohusiana na sekta ya madini, huku fedha hizo zikiwanufaisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini, wakiwemo wachimbaji wadogo, kampuni pamoja na watoa huduma.
Amesema NMB imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wadogo kupata mitaji kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu, pamoja na elimu ya fedha, mazingira na matumizi bora ya ardhi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali.
Ameongeza kuwa benki hiyo imezindua huduma ya SME Credit Card, inayowawezesha wafanyabiashara kupata mkopo wa hadi Sh milioni 50 bila riba kwa muda uliowekwa, na baada ya kurejesha fedha hizo wanaweza kuendelea kutumia huduma hiyo.
Amesema pamoja na mikopo, NMB inaendelea kutoa elimu ya fedha na ushauri kwa wadau wa sekta ya madini kupitia mipango mbalimbali ikiwemo NMB Business Club, huku wanawake wakinufaika na mpango wa NMB Orange Woman unaolenga kuwaongezea elimu ya fedha, ushauri na upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu.
Amesema wachimbaji wadogo wanaotaka kunufaika na huduma hizo wanapaswa kuwa na leseni halali za uchimbaji pamoja na kuzingatia vigezo vya kimazingira, kifedha na kibenki vinavyotakiwa katika upatikanaji wa mikopo.


Comments
Post a Comment