KATIBU MKUU WIZARA YA NISHATI NA MADINI ZANZIBAR ATEMBELEA BANDA LA GST KATIKA MAONYESHO YA 9 YA TEKNOLOJIA YA MADINI GEITA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Zanzibar, Ndugu Joseph Kilangi, ametembelea banda la Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) katika Maonyesho ya 9 ya Kitaifa ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Geita.
Katika ziara hiyo, Ndugu Kilangi ameongozwa na Kamishna wa Madini nchini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, ambaye amemueleza kuhusu majukumu, shughuli na huduma zinazotolewa na GST, hususan katika tafiti za kijiolojia na utafiti wa rasilimali madini nchini.
Akiwa katika banda hilo, Ndugu Kilangi amepata fursa ya kuona kwa vitendo teknolojia, vifaa na mbinu mbalimbali zinazotumika katika utafiti na uchunguzi wa madini. Aidha, amefahamishwa kuhusu huduma zinazotolewa na GST kwa wachimbaji, wawekezaji pamoja na wadau wengine wa Sekta ya Madini.
Ziara hiyo imefanyika wakati ambapo Maonyesho hayo ya 9 yanaendelea kuwakutanisha wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini kutoka maeneo tofauti, kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika utafutaji, uchimbaji na uchenjuaji wa madini nchini.
GST inaendelea kushiriki kikamilifu katika maonyesho hayo kwa kutoa elimu kwa wananchi, wachimbaji, wawekezaji na wadau wengine kuhusu huduma za utafiti wa kijiolojia na madini, pamoja na teknolojia zinazotumika katika kutambua, kuchunguza na kutathmini uwepo wa rasilimali madini nchini.
Ushiriki wa GST katika maonyesho hayo ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa tafiti za kijiolojia na matumizi ya teknolojia katika kuendeleza Sekta ya Madini nchini.










Comments
Post a Comment