Mkuu wa Wilaya ya Chato, Louis Peter Bura, amewataka wananchi kuacha tabia ya kusubiri umeme ukatike ndipo wakalalamike, bali washikamane na TANESCO kulinda miundombinu ya umeme kama mali yao.
Bura ametoa wito huo leo Septemba 29, 2026, mara baada ya kutembelea banda la TANESCO katika Maonesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Geita.
"Elimu ni muhimu. Mwananchi akiona nguzo imeegama, waya umeanguka, au mtu anachimba karibu na nguzo, atoe taarifa mapema. Kulinda miundombinu ya umeme ni kulinda maendeleo yetu," alisema Bura.
Amepongeza hatua ya TANESCO ya kidijitali ya kutumia vikundi vya mawasiliano vya WhatsApp na mifumo ya teknolojia ya mawasiliano ya kikanda. Amesema sasa mwananchi hahitaji kupanda daladala kufika ofisini, anawasilisha kero yake kwenye kundi na inatatuliwa haraka.
"Tangu kuanzishwa kwa makundi haya, malalamiko yamepungua kwa kiasi kikubwa. Hii ndiyo TANESCO tunayoitaka," alisema.
Katika angle nyingine, Bura ameunganisha suala la umeme na uhifadhi wa mazingira. Amesema taifa haliwezi kupiga hatua kama nishati ya kupikia bado ni kuni na mkaa unaotokana na ukataji miti hovyo.
"Ukataji miti unaleta jangwa. Serikali ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inahamasisha nishati safi, na TANESCO na REA wametuletea majawabu," alisema.
Akijibu wito huo, Afisa Huduma kwa Wateja Mkoa wa Geita, Lucas Sweet Sweke, amesema TANESCO imeleta suluhisho jikoni.
"Tumeleta majiko ya kisasa - Pressure Cooker na Induction*- yanayopika haraka, yanayotumia umeme kidogo na yasiyo na moshi. Ni fursa kwa mama wa Kichato, Geita na Tanzania nzima kuachana na kuni," alisema Sweke.
Amesema wananchi wanaotembelea banda la TANESCO maoneshoni wanapata elimu ya moja kwa moja na kuona majiko hayo yakifanya kazi.
Kwa mujibu wa viongozi hao, ulinzi wa nguzo moja ya umeme na matumizi ya jiko moja safi ni mchango mkubwa kuliko hotuba ndefu za mazingira.


Comments
Post a Comment