SERIKALI imeweka mkakati wa kupunguza muda ambao meli za mafuta hukaa bandarini, hatua inayolenga kuongeza ufanisi katika upokeaji na usambazaji wa mafuta pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji zinazoweza kuathiri bei kwa watumiaji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dk. James Mataragio, amesema hayo wakati wa ziara ya kukagua miundombinu ya mafuta katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Tanzania International Petroleum Reserves Limited (TIPER), jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali inalenga kuhakikisha meli zinazowasili nchini zinashusha mafuta kwa ufanisi na kuondoka bandarini kwa wakati, huku akisisitiza kuwa kila taasisi na mdau anayehusika katika mnyororo wa upokeaji na usambazaji wa mafuta anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa wakati.
“Ni matarajio ya Serikali kuona meli zikifika, zinashusha mafuta na kuondoka. Kila taasisi inapaswa kufahamu jukumu lake na kujipanga ipasavyo,” amesema Dk. Mataragio.
Amesema baadhi ya maghala binafsi yanakabiliwa na changamoto zinazohusiana na kasi ndogo ya kupokea na kuondosha mafuta, hali ambayo inaweza kuongeza muda wa meli kukaa bandarini na hivyo kuongeza gharama za uendeshaji.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Mataragio ameitaka Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kuimarisha usimamizi wa wamiliki wa maghala binafsi na kuhakikisha wanawekeza katika miundombinu yenye uwezo wa kuhudumia mahitaji ya soko kwa wakati.
Amesema wamiliki wa maghala wanapaswa kuboresha pampu na vifaa vya kupokea mafuta, hususan vile vilivyochakaa au visivyokuwa na uwezo unaokidhi mahitaji ya sasa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa PBPA, Erasto Simon, amesema taasisi hiyo itakutana na kampuni za mafuta (OMCs), TPA pamoja na wadau wengine kupitia mapitio ya Mwongozo wa Taratibu za Uendeshaji (SOP Manual).
Amesema mapitio hayo yanalenga kuweka wazi majukumu ya kila mdau, muda wa utekelezaji na uwajibikaji katika hatua mbalimbali za upokeaji, uhifadhi na usambazaji wa mafuta.
Hatua hiyo inatarajiwa kuimarisha ufanisi wa mfumo wa upokeaji na usambazaji wa mafuta nchini, kupunguza ucheleweshaji bandarini na kusaidia kudhibiti gharama zinazotokana na meli kukaa muda mrefu bila kuhudumiwa.

Comments
Post a Comment