Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema ushirikishwaji wa sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya Tanzania, hasa azma ya kufikisha thamani ya uchumi wa Taifa hadi dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo, Jumapili, Septemba 27, 2026, jijini Doha, Qatar, alipokutana na Makamu wa Kwanza wa Chama cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda cha Qatar (QCCI), Bw. Mohammed bin Ahmed bin Twar Al Kuwari, pamoja na ujumbe wake katika kikao kilichofanyika katika Hoteli ya Kempinski.
Waziri Mkuu amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuishirikisha sekta binafsi katika mipango ya maendeleo ya nchi, kupitia Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.
“Tunaamini kwamba Serikali peke yake haiwezi kufanikiwa katika uwekezaji huo bila kushirikisha wawekezaji wa ndani au wa nje. Ndiyo maana Serikali imeweka vivutio vya kiuwekezaji ili kuvutia mitaji,” amesema Dkt. Mwigulu.
Katika kikao hicho, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya uchumi na uwekezaji, pamoja na kuainisha fursa zilizopo Tanzania na Qatar, pamoja na fursa zinazotokana na ushiriki wa nchi hizo katika jumuiya za kikanda za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Baraza la Ushirikiano la Nchi za Kiarabu za Ghuba (GCC).
Aidha, kikao hicho kimekubaliana kuhusu umuhimu wa kuwakutanisha wafanyabiashara kutoka Tanzania na Qatar kupitia taasisi zao za uwakilishi, zikiwemo QCCI, TPSF na TCCIA, kwa lengo la kujadili kwa kina maeneo ya ushirikiano wa kimkakati, biashara na uwekezaji.
Kikao hicho kiliwashirikisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga; Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe; Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji; Wabunge pamoja na watendaji wengine wa Serikali.









Comments
Post a Comment