Benki ya Azania imeeleza kuwa inatoa huduma mbalimbali za mikopo kwa wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wa sekta ya madini, ikiwa ni pamoja na mikopo ya mitaji, uwekezaji na ununuzi wa mitambo na vifaa vya uzalishaji.
Kwa mujibu wa benki hiyo, baadhi ya mikopo hutolewa kwa ajili ya kuendesha shughuli za biashara na kulipwa kwa vipindi vya miezi mitatu, huku mikopo ya uwekezaji ikitolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Benki hiyo pia inatoa mikopo ya ununuzi wa mitambo na vifaa mbalimbali kwa ajili ya shughuli za uzalishaji, ikiwemo mashine, vifaa vya kutengeneza betri na vifaa vingine vya viwandani. Aidha, mikopo hutolewa kwa ajili ya ununuzi wa vyombo vya usafirishaji kama magari, malori na matipa.
Katika sekta ya madini, Benki ya Azania imeeleza kuwa ina bidhaa maalumu inayolenga kuwasaidia wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu wanaouza madini yao kupitia Benki Kuu ya Tanzania. Kupitia bidhaa hiyo, mteja anaweza kupata mkopo wa hadi Shilingi bilioni tano bila dhamana, kwa sharti la kutumia akaunti ya Benki ya Azania. Benki hiyo inaweza kutoa hadi asilimia 80 ya thamani ya fedha zinazotarajiwa kupokelewa.
Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wadau wa mnyororo wa thamani wa madini kuendelea na shughuli zao wakati wakisubiri kukamilika kwa taratibu za malipo.
Aidha, benki hiyo imesema imeingia makubaliano na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutoa mikopo yenye riba ya asilimia tano kwa mwaka kwa ajili ya ujenzi wa vituo na maeneo ya huduma za mafuta vijijini.
Kwa mujibu wa benki hiyo, huduma hiyo inalenga kusaidia kuongeza upatikanaji wa nishati na kuchochea uzalishaji katika maeneo ya vijijini, hususan yanayozunguka shughuli za uchimbaji madini.
Benki ya Azania pia inatoa mikopo ya uwekezaji ya muda mrefu, inayoweza kufikia miaka minane, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa, magari na mahitaji mengine yanayowawezesha wawekezaji katika sekta ya madini kuongeza uwezo wa uzalishaji na kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.

Comments
Post a Comment