Na Mwandishi wetu
Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Mkoa wa Shinyanga kimewahamasisha vijana na wachimbaji wadogo nchini kote kuchangamkia fursa ya mafunzo ya ukataji na ung'arishaji wa madini ya vito, hatua inayolenga kukuza uongezaji thamani ya rasilimali hizo hapa nchini.
Wito huo umetolewa na Mkufunzi wa Thamani ya Madini wa chuo hicho, Robert Onesmo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari katika Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita.
Onesmo amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha hakuna madini ghafi yanayosafirishwa nje ya nchi bila kuongezewa thamani.
Lengo kubwa ni kuongeza thamani ya madini yetu hapa hapa nchini kabla ya kusafirishwa au kuuzwa, ili nchi na wananchi wanufaike zaidi," amesema Onesmo.
Ameongeza kuwa chuo kinatoa mafunzo katika ngazi mbili ili kumwezesha kila mwenye nia kupata ujuzi kulingana na muda wake. Kozi ya kwanza ni Kozi Fupi (Short Course) inayochukua miezi miwili kwa wanaohitaji ujuzi wa haraka, na ya pili ni Kozi Ndefu (Long Course) inayochukua miaka miwili hadi mitatu kwa ujuzi wa kina na wa kitaalamu zaidi.
Akizungumzia ada za masomo, Onesmo amesema zimepangwa kwa gharama nafuu ili kuwawezesha vijana wengi kujiunga. Kwa mwanafunzi wa kutwa, ada ni Shilingi 60,000 kwa mwaka, huku mwanafunzi wa bweni akilipia Shilingi 120,000 kwa mwaka, kiasi kinachojumuisha malazi, chakula, matibabu, maji na umeme.
Onesmo ametoa wito kwa jamii, hususan vijana walioko mtaani na wachimbaji wadogo, kutumia fursa hiyo adhimu kupata elimu sahihi ya kutambua aina mbalimbali za madini na teknolojia ya kuyaongezea thamani, kwa manufaa ya kiuchumi na katika kufanikisha malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
Kwa upande wake, mwanafunzi wa chuo hicho, Daud John, amewataka vijana kuchangamkia fursa hiyo katika sekta ya madini hususan fani ya uongezaji thamani ya madini na kuacha kulalamika kuhusu ukosefu wa ajira.
Nasomea fani ya ukataji na ung'arishaji wa madini ya vito, tunafundishwa utambuzi wa madini, namna yanavyotokea asili na teknolojia ya kuongeza thamani kwa kuyakata na kuyang'arisha ili yawe tayari kuingia sokoni," amesema.
Ameongeza kuwa gharama za masomo ni nafuu sana na anapenda kuchukua nafasi hiyo kuwahamasisha vijana wenzake walioko mtaani kusomea kozi hiyo VETA Shinyanga.
Mwisho





Comments
Post a Comment