UKOSEFU WA MTAJI NA TEKNOLOJIA KUWAFANYA WACHIMBAJI WAONE LESENI KAMA MZIGO
Na Richard Mrusha
Umuhimu wa ushirikiano kati ya wachimbaji wadogo na watoaji wa msaada wa kiufundi (TSA) umeibuka wazi katika Siku ya Wachimbaji Wadogo iliyoadhimishwa Septemba 26, 2026 ndani ya Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.
Kupitia simulizi iliyosimuliwa na Emmanuel Francis Jirab kutoka Kampuni ya Yi Xing Kuangye Mining Co. Ltd, ilibainika jinsi ukosefu wa mtaji na teknolojia unavyoweza kumfanya mchimbaji aone leseni yake kama mzigo.
Jirab alieleza kuwa mchimbaji mmoja alifikia mahali pa kuandika barua kwenda Wizara ya Madini kuomba leseni zake zifutwe baada ya maduara yake kujaa maji na kushindwa kuendelea na shughuli kwa muda mrefu.
Wawekezaji walipokuja, walikuja wenyewe nyumbani, mimi sikuwatafuta. Wakatembelea na kukubali kwamba tutafanya nao uchimbaji," alisema Jirab akielezea namna wawekezaji kutoka China walivyojitokeza na kuingia makubaliano na mchimbaji huyo
Makubaliano hayo yalimlazimu mchimbaji huyo kukimbilia tena Wizarani kuzuia mchakato wa kufuta leseni zake, na sasa maeneo yaliyokuwa yamesimama yamerudi katika uzalishaji.
Kwa mujibu wa Jirab, mafanikio ya ushirikiano huo yameanza kuonekana sio tu mgodini bali hata katika maisha ya familia ya mchimbaji huyo ambaye sasa anamudu gharama za elimu ya mtoto wake anayesoma nje ya nchi.
Jirab alisema tukio hilo ni funzo kuwa changamoto za wachimbaji wadogo nyingi zinaweza kutatuliwa kama kutakuwa na ushirikiano wa karibu na wawekezaji wenye mtaji na teknolojia ya kisasa.
Mchimbaji huyo ameishukuru Serikali na Wizara ya Madini kwa kuweka mazingira wezeshi yanayowawezesha wachimbaji wadogo kunufaika na rasilimali za madini na kuvutia wawekezaji.
Siku ya Wachimbaji Wadogo na TSA imekuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wachimbaji, wawekezaji na watoa huduma za kiufundi ili kutafuta suluhu ya changamoto zinazowakabili.

Comments
Post a Comment