WAZIRI WA ULINZI NA JKT DKT. NYANSAHO AKAGUA UTENDAJI WA SHIRIKA LA NYUMBU, ASISITIZA KUONGEZA MCHANGO KATIKA UCHUMI
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Shirika la Tanzania Automotive Technology Centre (TATC), maarufu kama NYUMBU, lililopo Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, kwa lengo la kujionea utendaji wa shirika hilo na namna linavyotekeleza majukumu yake ya kimkakati.
Katika ziara hiyo, Waziri Nyansaho ametembelea maeneo mbalimbali ya shirika hilo linalomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), akipata fursa ya kuona shughuli zinazotekelezwa katika uzalishaji, ukarabati na ubunifu wa kiteknolojia, hususan katika sekta ya vyombo vya moto, vipuri na vifaa vya uhandisi.
Akizungumza na uongozi na menejimenti ya Shirika la NYUMBU, inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Luteni Jenerali na Balozi mstaafu Paul Meela, Waziri Nyansaho amesema ziara hiyo imelenga kupata uelewa wa kina kuhusu utendaji wa shirika, changamoto zinazolikabili pamoja na fursa zilizopo za kuongeza ufanisi na mchango wake katika maendeleo ya Taifa.
Amesema NYUMBU ni shirika la kimkakati lenye nafasi muhimu katika kusaidia shughuli za ulinzi na usalama, huku likiwa na uwezo wa kuchangia zaidi katika maendeleo ya teknolojia, uzalishaji wa ndani na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Waziri Nyansaho amepongeza uongozi na watendaji wa Shirika la NYUMBU kwa kazi wanazofanya, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia ipasavyo fursa zilizopo ili kuongeza uzalishaji, kuboresha huduma na kuhakikisha shirika hilo linaendelea kuwa sehemu muhimu ya juhudi za Serikali za kukuza uchumi na teknolojia nchini.
Aidha, amesisitiza kuwa taasisi za umma zinapaswa kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kutoa mchango unaoendana na matarajio ya Serikali katika kuimarisha uzalishaji wa ndani, ubunifu na utoaji wa huduma zenye manufaa kwa jamii.
Ziara hiyo pia ilihudhuriwa na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Salum Othman, wajumbe wa Bodi ya Shirika la NYUMBU, pamoja na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Makao Makuu ya JWTZ.
Tanzania Automotive Technology Centre (TATC), maarufu kama NYUMBU, ni shirika la umma lililo chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, linalojihusisha na shughuli mbalimbali za teknolojia ya magari na vifaa vya uhandisi, ikiwemo utengenezaji, ukarabati, ubunifu na uzalishaji wa vipuri na vifaa mbalimbali.
Shirika hilo limeendelea kuwa miongoni mwa taasisi muhimu katika kukuza uwezo wa ndani wa kiteknolojia na uhandisi, pamoja na kusaidia mahitaji ya kitaifa katika sekta zinazohitaji utaalamu na uzalishaji wa vifaa nchini.




Comments
Post a Comment