Dar es Salaam
Wafungwa zaidi ya 600 waliopo katika Gereza kuu Ukonga kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo katika kambi maalumu ya siku sita inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Kambi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa JKCI kusogeza huduma za kibingwa za moyo karibu na wananchi huku ikitambua kwamba afya ni haki ya kila binadamu na msingi muhimu wa maendeleo ya mtu na taifa kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kambi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema hii ni mara ya kwanza katika Serikali ya Awamu ya Sita kwa JKCI kufikisha huduma hizo za kibingwa katika mazingira ya gerezani.“Kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, badala ya kusubiri wananchi wenye changamoto za moyo kusafiri umbali mrefu kuifuata JKCI, imechukua hatua ya kuwafikia wananchi katika maeneo walipo ikiwemo wafungwa wa gereza la Ukonga”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema kambi hiyo ina umuhimu mkubwa kwa sababu inatambua kwamba kuwa mfungwa hakumvui mtu hadhi yake ya kuwa binadamu wala haki yake ya msingi ya kupata huduma za afya kwani wafungwa ni sehemu ya jamii na wanapohitaji huduma za afya wanapaswa kupata huduma hizo kwa kuzingatia utu, usawa na viwango vinavyokubalika.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza na Mkuu wa Kitengo cha Afya Nsajigwa Mwankenja aliushukuru uongozi wa JKCI kwa kulikumbuka kundi la wafungwa na kuwafikia kwaajili ya kuwafanyia uchunguzi wa afya kwani wanahitaji huduma hizo.
Kamisha Nsajigwa alisema wafungwa wakimaliza kutumikia kifungo huku wakiwa na afya duni watashindwa kulitumikia taifa kwa ukamilifu hivyo ni vyema kwa pamoja wakashirikiana na wadau kuhakikisha wafungwa wanapomaliza muda wa kutumikia adhabu zao wanatoka na afya njema ili waweze kushiriki katika majukumu ya ujenzi wa taifa wakiwa imara.“Wafungwa hawakai gerezani milele, wanapokuwa na afya njema kunakuwa na manufaa hata kwa jamii kwani wakitoka gerezani na maambukizi hasa ya magonjwa yanayoambukiza wanaweza kuiambukiza jamii pia”, alisema Kamishna Nsajigwa.
Kambi hiyo ya matibabu ni miongoni mwa kambi za matibabu zaidi ya 26 ambazo JKCI imezifanya katika mikoa Tabora, Kilimanjaro, Geita, Dar es Saalaam, Arusha, Mtwara, Lindi, Zanzibar, Dodoma, Iringa, Manyara, Bukoba, Pwani, Kigoma, Rukwa, Songea, Mwanza, Tanga, Mbeya, Singida pamo na katika makampuni mbalimbali nchini ambapo jumla ya watu 41,164 walifanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo
Hayo yamesemwa leo Agosti 11,2026,katika Gereza la Ukonga Jijini Dar es Salaam.

Comments
Post a Comment