Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Tamasha la Kizimkazi limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kutangaza utamaduni, utalii, biashara na fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar, sambamba na kuchochea maendeleo ya wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 12 Agosti 2026, alipokuwa akizindua rasmi Tamasha la Kizimkazi 2026 lenye kaulimbiu “KIZIMKAZI Kumenoga!” katika Mkoa wa Kusini Unguja.
Amepongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono ya kuasisi Tamasha hilo, ambalo limekuwa likichangia kuhifadhi mila na utamaduni, kukuza utalii na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kutumia Tamasha hilo kutangaza fursa za uwekezaji katika utalii, uvuvi, mwani na Uchumi wa Buluu, huku Serikali ikiendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji na miundombinu ya uzalishaji.
Amesema Tamasha la Kizimkazi linaunga mkono dhamira ya Serikali ya kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Zanzibar kutoka 800,000 hadi milioni 1.5, kupitia matukio maalum ya utalii na utangazaji wa vivutio, utamaduni, vyakula na ukarimu wa Wazanzibari.
Rais Dkt. Mwinyi amewapongeza waandaaji, wadhamini, taasisi za Serikali, Sekta Binafsi, wajasiriamali, wasanii, wanamichezo na wananchi kwa kufanikisha Tamasha la Kizimkazi 2026, akihimiza kuendelea kulitumia kama jukwaa la kufungua fursa mpya za maendeleo.
Tamasha hilo linaendelea hadi tarehe 14 Agosti 2026, ambapo kilele chake kitafanyika katika Uwanja wa Mwehe, Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja.























Comments
Post a Comment