Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wamiliki na waendeshaji wa mabasi ya mikoani yanayofanya shughuli za usafirishaji katika maeneo ya katikati ya jiji kurejesha huduma zao katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Magufuli, Ubungo, akiwapa hadi Jumatatu, Agosti 17, 2026, kutekeleza agizo hilo.
Chalamila amesema hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji, kurejesha utaratibu wa matumizi ya vituo rasmi vya mabasi na kuhakikisha fursa za kiuchumi zinawafikia pia watoa huduma wengine wa usafiri, wakiwemo waendesha daladala, mabasi ya mwendokasi, bajaji na bodaboda.
Amesema Dar es Salaam ina Stendi ya Magufuli iliyojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 80 na yenye uwezo wa kuhudumia mabasi mengi kwa wakati mmoja, hivyo hakuna sababu kwa mabasi makubwa ya mikoani kuendelea kuzagaa katika maeneo ya katikati ya jiji, ikiwemo Shekilango na maeneo yanayounganisha barabara kuelekea Magomeni.
“Stendi yetu ile imejengwa kwa zaidi ya bilioni 80. Ni stendi ambayo ni bora na pengine kuliko stendi yoyote Tanzania. Inaweza kuchukua magari mengi kwa pamoja. Lakini kwa bahati mbaya sana, mabasi mengi hayako pale,” amesema Chalamila.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, kuna kampuni sita zilizopewa vibali maalum vya kuendesha huduma za mabasi katika maeneo mengine ya jiji, ikiwemo kuwa na vituo vidogo katika maeneo yaliyokubaliwa, lakini kampuni ambazo hazina vibali hivyo hazipaswi kuendelea kutumia vituo vilivyo nje ya Stendi ya Magufuli.
“Wito wangu, kuanzia leo, Agosti 12, 2026, mpaka kufikia tarehe 17, wale wote ambao hawana vibali vya ku-operate stendi zao katikati ya mji, warudishe mabasi yao Ubungo, Stendi ya Magufuli,” amesema.
Agizo hilo linaendana na masharti yaliyowekwa katika Sheria Ndogo za Vituo vya Mabasi na Maegesho ya Vyombo vya Moto za Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo za mwaka 2022, ambazo zinaweka utaratibu wa matumizi ya vituo vya mabasi katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1) cha Sheria Ndogo hizo, Halmashauri ina wajibu wa kuanzisha vituo vya mabasi yanayofanya shughuli zake ndani ya eneo la Manispaa ya Ubungo, yakiwemo mabasi yanayotoka nje ya Halmashauri na yanayoingia ndani yake kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria na mizigo.
Aidha, Kifungu cha 6(1) kinaweka wajibu kwa kila mmiliki au msimamizi wa mabasi yanayotoka au kwenda mikoani na nchi jirani kuingia katika eneo lililotengwa na Halmashauri kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria na mizigo.
Sheria hiyo pia inaweka zuio kwa vituo visivyo rasmi, ambapo Kifungu cha 6(2) kinakataza mtu, mmiliki wa chombo cha usafiri au taasisi kuanzisha kituo cha mabasi, kupakia au kushusha abiria na mizigo katika eneo ambalo halijatengwa au kutambuliwa na Halmashauri kwa ajili ya shughuli hizo.
Hata hivyo, sheria inatambua uwepo wa vibali maalum, ambapo Kifungu cha 6(3) kinaeleza kuwa, isipokuwa kwa kibali maalum kutoka Halmashauri, mabasi yote yanatakiwa kuanza safari zake katika stendi iliyotengwa. Kifungu hicho ndicho kinachoeleza msingi wa tofauti kati ya kampuni zilizopewa ruhusa maalum na zile ambazo hazina kibali hicho.
Chalamila amesema mfumo unaokusudiwa ni mabasi makubwa ya mikoani kuishia Stendi ya Magufuli, kisha abiria wanaohitaji kwenda maeneo ya katikati ya jiji watumie huduma nyingine za usafiri zinazowaunganisha na maeneo wanayokwenda.
Amesema serikali tayari imeunganisha huduma ya Mwendokasi na Stendi ya Magufuli, hivyo abiria wanaweza kuendelea na safari zao kupitia usafiri wa mijini badala ya mabasi makubwa kuingia katikati ya jiji.
Amefananishia mfumo huo na usafiri wa anga, akisema abiria anayesafiri kwa ndege kwenda Kilimanjaro na kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro anaweza kutumia shuttle au usafiri mwingine kwenda Arusha au Moshi, badala ya ndege kuingia moja kwa moja katikati ya miji hiyo.
Kwa mantiki hiyo, Chalamila amesema mabasi makubwa yanapaswa kuwasafirisha abiria hadi Stendi ya Magufuli, ambako wanaweza kuunganisha safari zao kwa kutumia Mwendokasi, daladala, bajaji, bodaboda na huduma nyingine za usafiri.
Amesema kuendelea kwa mabasi makubwa kuingia katikati ya jiji kunaongeza foleni na wakati huohuo kuwaondolea fursa watoa huduma wengine wa usafiri ambao wanategemea abiria wanaoshuka katika vituo vikuu.
“Kitendo cha kuingiza mabasi katikati ya mji maana yake moja ni kusababisha foleni. Jambo la pili ni kunyang’anya fursa za bodaboda, bajaji, daladala, mwendokasi na kadhalika,” amesema.
Msimamo huo pia unaendana na Kifungu cha 6(7) cha Sheria Ndogo hizo, kinachokataza kufungua ofisi, kituo au kufanya biashara inayofanana na shughuli zinazofanywa katika kituo cha mabasi katika eneo lote la Halmashauri.
Sheria hizo pia zinaweka utaratibu wa maegesho ya vyombo vya usafiri. Kifungu cha 13(1) kinakataza kuegesha gari au chombo chochote cha usafiri katika maeneo ambayo hayajatengwa kwa ajili ya maegesho au kuegesha kwa namna isiyoruhusiwa.
Kwa mujibu wa masharti hayo, Halmashauri inaweza kukokota au kufunga chombo cha usafiri kilichoegeshwa isivyostahili na kumtaka mmiliki kulipa faini pamoja na gharama zinazohusiana na uvutaji na utunzaji wa chombo hicho.
Akizungumzia mabasi yanayohitaji kufanyiwa matengenezo, Chalamila amesema hakuna tatizo kwa mabasi kwenda gereji, lakini amesisitiza kuwa magari hayo hayapaswi kupaki au kufanyia matengenezo katika uso wa barabara kuu na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara.
Sheria Ndogo hizo pia zinaweka adhabu kwa wanaokiuka masharti yake. Kwa mujibu wa Kifungu cha 18, makosa yanayoweza kuchukuliwa hatua ni pamoja na kuegesha chombo cha usafiri katika eneo lisiloruhusiwa, kuingia katika kituo cha mabasi bila kulipa ushuru, kufanya shughuli zisizoruhusiwa na kuzuia maafisa au mawakala wa Halmashauri kutekeleza majukumu yao.
Aidha, Kifungu cha 19 kinaeleza kuwa mtu anayekiuka masharti ya Sheria Ndogo hizo, pale ambapo hakuna adhabu maalum iliyowekwa, anaweza kutozwa faini isiyopungua Sh 200,000 na isiyozidi Sh milioni moja, au kifungo kisichopungua miezi 12 na kisichozidi miezi 24, au adhabu zote mbili.
Kwa msingi huo, Chalamila amesema kuanzia Jumatatu, Agosti 17, 2026, serikali itaanza kuchukua hatua dhidi ya mabasi yatakayoendelea kutumia vituo visivyo na vibali, huku akiahidi pia kuweka wazi majina ya kampuni sita zilizopewa vibali maalum.
Amesema vibali hivyo vitakapomalizika havitaruhusiwa kuhuishwa, hatua ambayo inalenga kuhakikisha mabasi yote ya mikoani yanaanza na kumalizia safari katika Stendi ya Magufuli.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa Chalamila, inalenga kuweka mfumo mmoja unaoratibu usafiri wa mabasi ya mikoani na usafiri wa ndani ya jiji, kupunguza msongamano katika barabara za katikati ya Dar es Salaam na kuhakikisha miundombinu iliyowekezwa na Serikali inatumika kwa ufanisi, huku shughuli za usafirishaji zikifanyika kwa kuzingatia utaratibu na masharti ya kisheria yaliyowekwa na Halmashauri.




Comments
Post a Comment