MWaziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema Mkoa wa Mbeya na kwa ujumla Nyanda za Juu Kusini una uwezo mkubwa wa kuongeza mchango wake katika uchumi wa Tanzania, akisisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji, kuchakata mazao na kuimarisha uwekezaji katika viwanda.
Mhe. Balozi Omar ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani Mbeya, ambapo alitembelea Ofisi za Mkoa za Chama cha Mapinduzi (CCM), jijini Mbeya.
Amesema Nyanda za Juu Kusini zinachukua takribani asilimia 20 ya eneo lote la Tanzania, lakini mchango wake katika Pato la Taifa bado haujaakisi kikamilifu ukubwa wa eneo hilo na utajiri wa fursa zilizopo.
Amesema hali hiyo inatoa nafasi kwa Serikali, sekta binafsi na wadau wengine kuongeza uwekezaji katika kilimo, madini, viwanda na sekta nyingine za uzalishaji ili kuongeza tija na mapato ya wananchi pamoja na Taifa kwa ujumla.
“Bado tuna fursa kubwa sana ya kuimarisha mchango wetu katika pato la Taifa uendane na eneo tulilonalo, na si kwa sababu hatuna fursa,” amesema Mhe. Balozi Omar.
Aitaka Tanzania kuongeza thamani ya mazao
Waziri Balozi Omar amesema Tanzania haiwezi kunufaika kikamilifu na rasilimali zake iwapo itaendelea kuzalisha mazao na kuyauza bila kuyaongezea thamani.
Amesema Serikali itaendelea kuweka msisitizo katika kujenga na kuimarisha mnyororo wa thamani, hususan kwa kuhakikisha mazao yanayozalishwa nchini yanachakatwa hapa hapa kabla ya kuuzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Msisitizo wetu uwe kwenye mnyororo wa thamani. Tunaweza kulima, kuvuna na kuuza mazao, lakini tunahitaji kuwa sehemu kubwa zaidi ya mnyororo wa thamani kwa kuhakikisha uchakataji unafanyika hapa nchini,” amesema.
Amesema kuongeza viwanda vya kuchakata mazao kutasaidia kuongeza ajira, kipato cha wakulima na mapato ya Serikali, sambamba na kuchochea ukuaji wa viwanda na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Akizungumzia nafasi ya Mbeya katika uchumi wa Taifa, Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe. Patrick Mwalunenge, amesema mkoa huo una uwezo mkubwa wa kuwa kitovu cha uzalishaji, biashara na uchakataji wa mazao kwa Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani.
Amesema Mbeya ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayozalisha mazao ya biashara kama chai, kahawa na kakao, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha masoko ya wakulima na kuvutia uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao hayo.
Mhe. Mwalunenge ameitaka Serikali kuendelea kuimarisha miundombinu ya biashara na viwanda, ikiwemo ujenzi wa bandari kavu na kongani za viwanda, ili kuongeza thamani ya uzalishaji na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kwenda katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Amesema nafasi ya kijiografia ya Mbeya, ikiunganishwa na uwezo mkubwa wa uzalishaji wa kilimo katika Nyanda za Juu Kusini, inatoa fursa ya kuunganisha kwa ufanisi uzalishaji, uchakataji, usafirishaji na masoko.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Lupa-Chunya, Mhe. Masache Kasaka, amesema Chunya ina mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa kupitia uzalishaji wa dhahabu na tumbaku.
Amesema wilaya hiyo inaongoza kwa uzalishaji wa dhahabu miongoni mwa wachimbaji wadogo nchini, ikiwa na uzalishaji wa wastani wa kilo 400 za dhahabu kwa mwezi.
Amesema changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo ya uzalishaji ikitatuliwa, itasaidia kuongeza tija katika uchimbaji wa dhahabu na kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi.
“Chunya ina fursa kubwa katika uzalishaji wa tumbaku. Kama kutaimarishwa kwa miundombinu ya umeme, maji na barabara, pamoja na kukamilishwa kwa miradi inayotekelezwa, kutasaidia wananchi kutumia kikamilifu fursa zilizopo katika sekta za uzalishaji,” amesema Mhe. Kasaka.
Wakati huohuo, Mhe. Balozi Omar amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha shughuli za uchimbaji wa madini mkoani Mbeya zinafanyika kwa kuzingatia usalama wa afya za wachimbaji, wananchi na utunzaji wa mazingira.
Amesema Serikali inatambua mchango wa madini katika uchumi, lakini shughuli hizo zinapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia kanuni zinazolinda maisha ya watu na mazingira.
Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuboresha mazingira ya uzalishaji, ikiwemo miundombinu ya umeme, ili kuwezesha sekta ya madini na sekta nyingine za uzalishaji kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.
Msisitizo uliotolewa na Waziri wa Fedha unaweka Mbeya na Nyanda za Juu Kusini katika nafasi muhimu ya kuongeza kasi ya uchumi kupitia uzalishaji wenye tija, kuongeza thamani ya mazao, viwanda, madini na biashara, huku ukilenga kuhakikisha wananchi wananufaika zaidi na fursa zinazopatikana katika eneo hilo.

Comments
Post a Comment