Na Mwandishi wetu
Katika kipindi kifupi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeandika mafanikio makubwa ambayo yamekuwa mfano wa kuigwa katika sekta ya hifadhi ya jamii nchini.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, alipotembelea banda la PSSSF katika Maonesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Waziri Sangu amesema thamani ya mfuko huo imekua kwa kasi ya ajabu kutoka Shilingi Trilioni 7.4 wakati Rais Samia anaingia madarakani, hadi kufikia Shilingi Trilioni 16.96 kwa sasa.
Amesema ongezeko hilo la zaidi ya mara mbili linathibitisha uthabiti, uwazi na usimamizi bora wa fedha za wanachama na wastaafu.
Kwa mujibu wa Waziri Sangu, mafanikio ya PSSSF hayaishii kwenye ukuaji wa mitaji pekee, bali pia kwenye ubora wa huduma.
Amesema kupitia kaulimbiu maarufu ya "Tunalipa Jana", PSSSF sasa inahakikisha fao la mstaafu linalipwa kwa wakati bila urasimu wala kuzungushwa, huku pensheni ya kila mwezi ikilipwa kabla ya tarehe 25 – jambo lililowarejeshea matumaini maelfu ya wastaafu nchini
Katika hatua nyingine inayogusa moja kwa moja maisha ya wastaafu, kima cha chini cha pensheni kimeongezeka kutoka Shilingi 100,000 hadi Shilingi 250,000 kwa mwezi.
Waziri amesema ongezeko hilo la asilimia 150 limeondoa machozi kwa wastaafu wa kada za chini na kurejesha heshima na thamani ya utumishi wa umma.
Zamani mstaafu kutoka Kakonko au Chato ilimlazimu kusafiri hadi Dar es Salaam au Dodoma kwa ajili ya uhakiki. Leo, mateso hayo yamebakia historia.
PSSSF imeboresha mifumo yake ya TEHAMA, na sasa mstaafu anaweza kuhakikiwa akiwa popote alipo – kwa njia ya kidijitali, kwa haraka na bila gharama yoyote.
Mbali na maboresho ya malipo na mifumo, PSSSF pia imewekeza katika utoaji wa elimu kwa kushirikiana na waajiri kote nchini.
Lengo ni kuwaandaa watumishi kisaikolojia na kiuchumi kabla ya kustaafu, ili maisha yao ya baada ya utumishi yawe mwanzo mpya wenye matumaini, na si mwisho wa safari.
Kwa hakika, PSSSF imejidhihirisha kuwa nguzo imara ya ustawi wa mtumishi wa umma, akiwa kazini na hata baada ya kustaafu.

Comments
Post a Comment