Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Salome Kessy, amewataka wanamichezo wanaoiwakilisha Wizara katika Michezo ya SHIMIWI 2026 mjini Moshi kuzingatia nidhamu, uwajibikaji na maadili ya Utumishi wa Umma, akisisitiza kuwa kila mmoja abebe taswira ya Wizara katika kipindi chote cha mashindano.
Bi. Kessy ameyasema hayo Septemba 18, 2026 jijini Dodom akizungumza na wanamichezo watakaoshiriki michezo inayotarajiwa kufanyika mkoani Kikimanjaro kuanzia Septemba 20 hadi Oktoba 7, 2026.
Ameongeza kuwa, mafanikio katika michezo hayawezi kutenganishwa na nidhamu, akiwataka wanamichezo kutunza utimamu wa miili yao, kuzingatia ushauri wa madaktari, kula vizuri na kupumzika kwa wakati badala ya kutumia muda wa mapumziko kuzurura.
Aidha, amewataka viongozi na walimu wa timu kuhakikisha kila mchezaji anatumika ipasavyo kulingana na uwezo wake, huku akisisitiza kuwa vitendo vya utovu wa nidhamu havitavumiliwa na hatua stahiki zichukuliwe kwa watakaokiuka taratibu za timu na maadili ya Utumishi wa Umma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Michezo ya Wizara ya Ardhi Bw. Swagile Msananga ameishukuru Wizara kwa kuweka mazingira mazuri ya maandalizi ya timu, ambapo wanamichezo wamefanya mazoezi kwa zaidi ya mwezi mmoja sambamba na kushiriki mabonanza matatu pamoja na michezo ya majaribio, hatua aliyoieleza kuwa inaenda kusaidia timu kupata ushindani na kujiimarisha kuelekea SHIMIWI.
Ameeleza kuwa katika mabonanza hayo, timu ya Kuvuta Kamba Wanawake na timu ya Mpira wa Miguu zilifanikiwa kutwaa vikombe viwili, jambo alilolitaja kuwa ni ishara ya maandalizi mazuri na kusisitiza kuwa, wanamichezo hao wanaenda kutumia uzoefu huo kuongeza juhudi katika mashindano hayo.
Jumla ya wanamichezo 96 wanaiwakilisha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazikatika michezo ya mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta kamba, riadha, karata, bao, kurusha tufe, darts na draft huku kauli mbiu ya SHIMIWI ikisema "Watumishi wa Umma Tuko Tayari Kwa Afcon 2027"









Comments
Post a Comment