Na Mwandishi wetu
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeandika mafanikio makubwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, baada ya thamani yake kupaa hadi Shilingi Trilioni 11.5 kutoka Trilioni 5.7 mwaka 2022
Takwimu hizo zimetajwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, alipotembelea banda la NSSF katika Maonesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Amesema Mfuko ulikua kutoka Trilioni 5.7 mwaka 2022, hadi Trilioni 10.4 Desemba mwaka jana, na sasa Trilioni 11.5, huku ukitarajia kuvuka Trilioni 12 ifikapo Desemba 2026,
Mafanikio hayo yanatokana na usimamizi bora na Mpango Mkakati mpya wa Miaka Mitano unaolenga kufikisha Mfuko hadi Trilioni 24 ifikapo 2031.
Waziri Sangu amesema ukuaji huo unadhihirisha kuwa NSSF imejipanga kuhudumia Sekta Binafsi ambayo ndiyo injini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuchangia asilimia 70 ya utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Msemaji Mkuu wa NSSF, Lulu Mengele, amethibitisha mafanikio hayo, akisema kuongezeka kwa thamani ya Mfuko kutoka Trilioni 5.7 hadi Trilioni 11.5 ni matokeo ya mikakati madhubuti ya uwekezaji na uandikishaji wa wanachama wapya kupitia mpango wa Hifadhi Scheme unaolenga wachimbaji wadogo, bodaboda na mama lishe.



Comments
Post a Comment