Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imefanikiwa kununua zaidi tani 30 za dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa walio rasmi, hatua ambayo imechangia kuongeza akiba ya fedha za kigeni ya nchi kwa takribani Dola za Marekani bilioni 2.05.
Akizungumza kuhusu mpango huo na waandishi wa habari Septemba 25,2026 katika Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini kwenye viwanja Vya Dkt.Samia Suluhu Hassan mkoani Geita, Mchambuzi wa Fedha Mwandamizi kutoka BoT, Idara ya Masoko ya Fedha za Nje, Glory Gabriel Maembe, amesema mpango wa Benki Kuu wa kununua dhahabu nchini umetekelezwa kwa takribani miaka miwili kwa lengo la kuongeza akiba ya fedha za kigeni.
Kwa mujibu wa Maembe, ununuzi huo umewezesha BoT kupata kiasi kikubwa cha dhahabu kutoka ndani ya nchi na hivyo kuongeza mchango wa sekta ya madini katika kuimarisha akiba ya taifa ya fedha za nchi.
Mbali na kuongeza akiba hiyo, mpango huo umeendelea kutoa soko la uhakika kwa wachimbaji wa dhahabu nchini, huku ukichochea urasimishaji wa shughuli za uchimbaji madini.
Aidha, mpango huo umechangia kukuza viwanda vya ndani vya kusafisha dhahabu (local refineries), hatua inayolenga kuongeza thamani ya madini yanayozalishwa nchini kabla ya kuuzwa katika masoko ya ndani na nje.
Katika kuboresha mazingira ya biashara kwa wachimbaji, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kupunguza gharama zinazohusiana na biashara ya dhahabu. Miongoni mwa hatua hizo ni kupunguza kiwango cha mrabaha kutoka asilimia sita hadi asilimia nne, kuondoa ada ya ukaguzi ya asilimia moja pamoja na msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika mazingira yaliyowekwa na mamlaka husika.
Maembe amesema pia malipo kwa wauzaji wa dhahabu yameboreshwa, ambapo yanalenga kufanyika kwa haraka na ndani ya muda usiozidi saa 24.
Hatua hizo zinaendelea kuifanya sekta ya dhahabu kuwa sehemu muhimu katika kuongeza mapato ya nchi, kuimarisha akiba ya fedha za kigeni na kuboresha mazingira ya shughuli za uchimbaji na biashara ya madini nchini.


Comments
Post a Comment