Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wananchi hususan wakulima , wafugaji na wavuvi kuchangamkia fursa zinazotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kukuza mitaji ya biashara zao.
Ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Benki ya maendeleo ya kilimo Kanda ya Zanzibar Afisini kwake Vuga.
Amesema Benki ya maendeleo ya Kilimo ina mchango mkubwa katika kuwawezesha kifedha na kuwapatia ujuzi wa kisasa wakulima, wafugaji na wavuvi ili waweze kukuza mitaji yao hivyo TADB wanapaswa kufikisha elimu kwa wananchi ili waweze kutambua fursa za kilimo na ufugaji zinazopatikana kupitia benki ya maendeleo ya Kilimo.
Aidha, Mhe. Hemed amesema wananchi wengi bado hawajaziona fursa za uwekezaji wa Kilimo zinazopatikana Zanzibar hasa vijijini ambako kuna maeneo mengi ya kufanya uwekazi endelevu na stahmilivu wa Kilimo.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka viongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Kanda ya zanzibar kuhakikisha wanawafikia wananchi katika kuwapatia elimu ya ukulima, ufugaji na uvuvi ili waweze kulima kilimo chenye tija pamoja na kuwataka kuitumia Kilimo TV na vyombo nyengine vya habari katika kufikisha taaluma hiyo.
Kwa upande wake Meneja wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Kanda ya Zanzibar Bwana ALLY JAMAL amesema jukumu kubwa la benki ya Kilimo ni kutoa mikopo nafuu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ambapo kwa kipindi cha miaka miwili zaidi ya Shilingi Bilioni 15 zimeshawanufaisha wananchi wa Zanzibar hususan vijana na wananwake wanajishughulisha na shughuli za kilimo.
JAMAL amesema ili wananchi waweze kufuga na kulima kilimo endelevu chenye tija Benki ya Kilimo imejipanga kuwafikia wananchi kuwapatia elimu juu ya matumizi ya fedha katika kuekeza kwenye kilimo lakini pia kuwapa ujuzi na maarifa juu ya namna bora ya kulima kilimo jumuishi ambacho kitakamilisha ndoto zao.
JAMAL amesema mafanikio yaliyopatikana katika kipindi kifupi tangu kufunguliwa kwa benki hio hapa Zanzibar ni pamoja na kuwafikia wakulima, wafugani na wavuvi wengi Unguja na Pemba ambao kupitia fursa za TADB wameweza kujiajiri na kuzalisha ajira kwa vijana wengi hivyo amewataka wananchi hasa vijana kuzitumia fursa hizo kwa maendeleo ya sekta ya kilimo Zanzibar.


Comments
Post a Comment