Na Mwandishi wetu Jovina Massano,Musoma.
MABORESHO na mazingira rafiki kwa wawekezaji na wafanyabiashara hapa nchini yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita yazidi kuchochea Maendeleo nchini.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Suguti View Hotel Masegenya John Chiganga mara baada ya kuzinduliwa na kuwekwa kwa jiwe la msingi katika hotel hiyo na Kiongozi wa mbio za mwenge ndugu Wazo Michael Mwang'onda akiwa na wakimbiza Mwenge wa uhuru kitaifa.
Amesema uwepo wa miundombinu muhimu maeneo ya vijijini kunazidi kuwavutia wawekezaji na wafanyabiashara na kuzidi kuchochea Maendeleo yanayokwenda kuongeza vipato vya wananchi wengi na kukuza uchumi kwa jamii na Serikali.
Amefafanua kuwa Uwekezaji huo umegharimu kiasi cha Shillingi za kitanzania zaidi ya million 100.17 zikiwa zimetokana na biashara ya uvuvi katika ziwa Victoria.
Mradi huo umewezesha baadhi ya jamii katika kijiji Cha Suguti kupata soko la uuzaji wa bidhaa za mazao ya nafaka na uvuvi katika eneo hilo.
Sanjari na hayo pia mradi huo umesogeza huduma za kitalii na maradhi kwa wageni na kuwezesha jamii iliyopo katika kijiji hicho kupata ajira na kuongeza mapato kwa Serikali na jamii pia.
Hakusita kutoa pongezi na shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele kwa kuendelea kuweka na kuboresha mazingira rafiki kwa wawekezaji na wafanyabiashara kunakopelekea kuzidi kuongeza wigo wa biashara maeneo ya vijijini.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi mkoa wa Mara wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) mfalme Julius Masubo Kambarage amesema Mwenge ni kichocheo cha Maendeleo kwa watu wote bila kujali itikadi za vyama.
Ameikumbusha jamii umuhimu wa mwenge wa uhuru na misingi yake tangu kuanzishwa kwake Mwaka 1964 ulipoasisiwa na Hayati Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere.
Ameeleza kuwa Lengo kuu la mwenge wa uhuru ni kuleta Amani, Upendo na kuondoa chuki na fitina miongoni mwa watanzania.
"Hivi Sasa mwenge wa Uhuru ni kichocheo cha Maendeleo ambapo unakwenda kufungua miradi mbalimbali ambayo inatoa huduma kwa jamii na wananchi wanatakiwa kuwa walinzi wakuu wa miradi hiyo kwa kuwa inawahidumia",amesema Mfalme Masubo.
Amesisitiza uwepo uangalizi mzuri wa miradi hiyo na kuiasa jamii kuwa sehemu ya kuitunza miundombinu hiyo kwa Maendeleo endelevu kwa kuwa ipo kwenye maeneo yao.
Amewakumbusha wananchi kuwa mwenge wa uhuru si wa kisiasa ni wa watanzania wote kwa kuwa unakwenda kufungua miradi ya maendeleo ya afya, elimu, miundombinu ya barabara, maji,viwanda na kilimo.
Akimalizia Mkurugenzi msaidizi wa Suguti View hotel Happiness Masatu kwa kuwashukuru wananchi wa kijiji Cha Suguti Ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri ya Musoma vijijini, Ofisi ya mkuu wa Wilaya na Mkoa kwa kuweza kuwapokea na kushirikiana katika uanzishaji wa mradi huo.
Amewaomba na kuwasihi Vijana kuwa na uthubutu na nidhamu ili kufikia malengo kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo na kujipatia kipato na kukuza uchumi.
"Uthubutu wa Vijana utaongeza upatikanaji wa ajira kwa wengine na kuchochea Maendeleo katika eneo husika,Vijana ni nguvukazi ya Taifa tukipambana tutainua nchi yetu", amesema Happiness.
Pia amewaasa Vijana wa kike kutojihusisha na biashara zinazoutweza utu wao na badala yake wawe wapambanaji kwa kujifunza shughuli mbalimbali na kupata vipato vyenye kukidhi mahitaji yao huku akitoa mfano wa biashara za uuzaji karanga,maandazi,chapati mbogamboga na matunda ambayo mtaji wake ni mdogo.
Amewashauri pia Vijana kuwa na uvumilivu katika utafutaji wa kutokata tamaa kwani uvumilivu huleta matokeo chanja na kuleta mafanikio kutokuwa tayari kujiingiza katika makundi yasiyofaa ya matumizi ya madawa ya kulevya.



Comments
Post a Comment