Serikali mkoani Mara imiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuanzisha Mamlaka ya Uhifadhi wa ziwa Victoria hatua ambayo itasaidia uhifadhi na uendelevu wa ziwa hilo ambalo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa mkoa na watu wake.
Ombi hilo limetolewa mjii Musoma leo Jumanne Agosti 11 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Bashiru Ally ambaye yupo mkoani Mara kwa ziara ya siku nne.
Kanali Mtambi amesema kutokana na shughuli za kiuchumi na kijamii zinazofanywa ndani ya ziwa hilo ipo haja ya kuwa na mamlaka maalumu itakayokuwa inasimamia ziwa hilo ili shughuli hizo ziweze kufanyika kwa ufanisi na kuleta tija zaidi bila kuathiri uhai wake.
Ametolea mfano suala la ufugaji wa vizimba ambalo limepata mapokeo makubwa mkoani Mara baada ya Serikali kuanza kuwezesha wavuvi ambapo amesema vijana wengi hivi sasa wameamua kujiajiri kupitia ufugaji huo ndani ya ziwa hilo hivyo ipo haja ya kuwa na mamlaka rasmi itakayosimamia rasilimali hiyo muhimu.
"Kuhusu gharama za uendeshaji hili sio tatizo kwani mamlaka hiyo itakuwa na uwezo wa kujiendesha yenyewe kama zilivyo mamlaka zingine kikubwa tuwe na chombo ramsi kwaajili ya kusimamia hii rasilimali yetu muhimu," amesema
Amesema licha ya ziwa hilo kuwa kichocheo muhimu kwa ukuaji wa uchumi bado linakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinatishia uhai wake hivyo ni vema kuwa na chombo maalumu kitakaosimamia na kupanga namna nzuri ya kufanya shughuli za kiuchumi ndani ya ziwa hilo.
Kanali Mtambi pia ameomba uimarishaji wa sekta ya mifugo hususan kusaidia upatikanaji wa mbegu bora za kisasa ili kuwasaidia wafugaji waweze kufuga kisasa ufugaji wenye tija.
Amesema licha ya mkoa wa Mara kuwa na mifugo mingi bado wafugaji hawajapata tija kutokana na kuwa na mbegu za asili.
"Tunaomba tupate mbegu bora zile mbegu ambazo mfugaji atapata tija kwa muda mfupi mfano kuna wale ng'ombe ana miezi tisa lakini anakuwa na kilo 1,000 tofauti na hawa tulionao ambapo ng'ombe ana miaka mitatu hadi mitano lakini hawezi kufikisha kilo 1,000," amesema
Amesema suala la uanzishwaji na ufufuaji wa viwanda hasa vya kuchakata mazao ya mifugo pia ni la muhimu kwani litasaidia kuboresha mnyororo wa thamani katika sekta ya mifugo.
"Viwanda vitasaidia kuongeza thamani ya mazao ya mifugo kama nyama, maziwa na ngozi tunaomba hili nalo lipewe kipaumbele na wizara ili maendeleo yaweze kuwagusa wananchi moja kwa moja," amesema
Akizungumza kuhusu maombi hayo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Bashiru Ally amesema tayari maombi hayo yaneanza kufanyiwa kazi lengo likiwa ni kuboresha na kuimarisha sekta za uzalishaji ili kuboresha uchumi wa wananchi ikiwa ni pia ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025/50.
"Tuna kituo cha kupandikiza mbegu bora za mifugo kule Arusha na tuna mpango wa kuanza kufungua matawi sehemu mbali mbali nchini ili mbegu hizo ziweze kupatikana kwa urahisi kwa wafugaji ili waweze kufanya ufugaji wenye tija," amesema
Kuhusu mamlaka ya usimamizi wa ziwa Victoria, Waziri Bashiru amesema Wizara yake iko katika hatua nzuri ya uanzishwaji wa mamlaka ya kuhifadhi na kusimamia sekta ya uvuvi hatua ambayo pia itasaidia kulinda maliasili za nchi sambamba na kuboresha shughuli za uvuvi.
Katika hatua nyingine, Waziri Bashiru amaeupongeza uongozi mkoa wa Mara kwa namna ulivyofanya uhamasishaji ambao umewezesha vijana wengi kuomba mkopo kufuatia Serikali kutenga Sh200 bilioni kwaajili ya mikopo kwa vijana.
Amesema mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa iliyoongoza kwa kutuma maombi mengi ya mikopo hiyo ingawa hakutoa takwimu huku akitoa wito kwa wakuu wa mikoa mingine kuiga mfano huo wa mkoa wa Mara ili vijana wengi waweze kuomba mikopo hiyo.
"Kwakweli maombi kutoka Mara ni mengi mno,Mara mmefanya vizuri sana,lakini kuna baadhi ya mikoa maombi ni machache sana hadi tunafikiria kuanza mchakato upya,nawaagiza wakuu wa mikoa wengine kujifunza kwa mkoa huu," amesema.





Comments
Post a Comment