Na Dawati la Habari Polisi;Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura, kwa hatua ya kuirejesha timu ya Polisi Tanzania katika Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/2027.
Mhe. Mtanda ametoa pongezi hizo leo Agosti 9, 2026, wakati akifungua rasmi Mashindano ya Polisi Jamii Cup Kanda Namba 7 yanayofanyika katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Amesema kurejea kwa Polisi Tanzania katika Ligi Kuu ni hatua muhimu inayopaswa kuungwa mkono, huku akisisitiza umuhimu wa michezo katika kuimarisha mahusiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.
“Nitumie nafasi hii kumpongeza IGP Camillus Wambura kwa hatua ya kuirejesha timu ya Polisi Tanzania katika Ligi Kuu ya NBC. Hii ni hatua nzuri na muhimu kwa Jeshi la Polisi na tunapaswa kuiunga mkono timu yetu ili iweze kufanya vizuri,” alisema Mtanda.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema michezo ni kiungo muhimu katika kujenga uaminifu, umoja na mshikamano kati ya Jeshi la Polisi na jamii, akiwataka wachezaji na washiriki wa mashindano hayo kuzingatia nidhamu.
“Michezo inatuunganisha. Ni fursa ya kujenga uaminifu na ushirikiano kati ya Polisi na wananchi. Kwa hiyo, ni muhimu washiriki wote kudumisha nidhamu, umoja na mshikamano katika kipindi chote cha mashindano,” alisema.
Mashindano ya Polisi Jamii Cup Kanda Namba 7 yamepangwa kufanyika kwa siku mbili na yamewashirikisha zaidi ya wanamichezo 250 kutoka mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Mara pamoja na Tarime na Rorya.
Mashindano hayo yanalenga kupata zaidi ya wachezaji 90 watakaounda timu ya Kanda Namba 7, ambayo itaiwakilisha kanda hiyo katika mashindano ya kitaifa yatakayofanyika jijini Mbeya Agosti 25, 2026.
Mashindano ya kitaifa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Polisi Jamii nchini, yenye kauli mbiu:
“Miaka 20 ya Polisi Jamii: Jamii na Polisi kwa Pamoja Katika Kuzuia Uhalifu, Kudumisha Amani na Usalama wa Taifa.”
Kauli mbiu hiyo inalenga kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya wananchi, wadau na Jeshi la Polisi katika kubaini na kuzuia uhalifu mapema, kwa lengo la kulinda amani, utulivu na usalama unaochochea maendeleo endelevu ya taifa.
Kwa upande wake, Afisa Mnadhimu wa Mkoa wa Mwanza, ACP Florence Mwenda, amesema mashindano hayo kwa upande wa Mkoa wa Mwanza yanatarajiwa kufanyika wilayani Kwimba katika tarehe iliyopangwa.
“Kwa upande wa Mkoa wa Mwanza, mashindano haya yanatarajiwa kufanyika wilayani Kwimba kama ilivyopangwa, na maandalizi yanaendelea kuhakikisha tunapata timu bora ya kuwakilisha mkoa,” amesema ACP Mwenda.
Naye Afisa Polisi Jamii Mkoa wa Simiyu, ACP Ochieng Asiago, amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa kushiriki katika ufunguzi wa mashindano hayo, akibainisha kuwa michezo mbalimbali inatarajiwa kuchezwa.
“Tunamshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kufungua mashindano haya. Michezo itakayochezwa ni pamoja na mpira wa miguu, kuvuta kamba na netiboli. Lengo kubwa ni kuimarisha ushirikiano na mahusiano mazuri kati ya Polisi na wananchi,” amesema ACP Asiago.
Mashindano ya Polisi Jamii Cup Kanda Namba 7 ni sehemu ya juhudi za Jeshi la Polisi kutumia michezo kama nyenzo ya kuimarisha ushirikiano na wananchi katika kuzuia uhalifu, kudumisha amani na usalama wa taifa.










Comments
Post a Comment