Na Angela Sebastian,Kyerwa
Ushirikiano wa karibu kati ya wazazi, walezi, walimu na viongozi umeelezwa kuwa chachu ya mafanikio makubwa ya kielimu katika Shule ya Sekondari Kimuli, iliyopo Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, baada ya shule hiyo kufanya vizuri katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita mwaka 2026.
Shule hiyo imeibuka ya kwanza kwa shule za Serikali mkoani Kagera, ya pili kwa shule zote za mkoa huo na kushika nafasi ya 27 kitaifa, baada ya wanafunzi wote 65 waliofanya mtihani huo kupata Daraja la Kwanza.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kimuli, Daniel Kifigo, alisema hayo wakati wa hafla ya kuwapongeza na kuwakabidhi tuzo na zawadi walimu pamoja na shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya Taifa wilayani Kyerwa.
Kifigo alisema mafanikio hayo yamepatikana licha ya shule hiyo kukabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa maji safi na salama, hali inayowalazimu wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata maji.
Alisema wanafunzi hao hutumia takribani saa nne kwenda na kurudi kutafuta maji, lakini changamoto hiyo haikuwazuia kufanya vizuri katika mitihani yao.
“Darasa lilikuwa na wanafunzi 65 na wote wamepata Daraja la Kwanza,hii imeifanya shule yetu kushika nafasi ya kwanza wilayani, ya pili kimkoa kwa shule zote na ya kwanza kwa shule za Serikali mkoani Kagera. Kitaifa tumeshika nafasi ya 27,” alisema Kifigo.
Kwa mujibu wa Kifigo, mafanikio hayo yametokana na umoja, bidii na uwajibikaji wa walimu, wazazi, wanafunzi pamoja na viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya Kata hadi Wilaya.
Alisema walimu wamekuwa wakijitoa kwa moyo wote, huku wazazi wakitoa ushirikiano mkubwa kwa kuchangia kwa hali na mali pale shule inapohitaji msaada kwa ajili ya maendeleo ya wanafunzi.
“Tunawashukuru sana wazazi kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha hili. Wamekuwa wakituunga mkono kwa hali na mali pale tunapowahitaji. Wakati mwingine wamechangia hata chakula inapobidi,” alisema.
Aliongeza kuwa upatikanaji wa mahitaji muhimu, ikiwemo chakula, umewasaidia wanafunzi kusoma kwa utulivu na kujiamini bila kuwa na mawazo yanayoweza kuathiri masomo yao.
“Mwanafunzi anapopata mahitaji yake muhimu kwa wakati, anasoma kwa kujiamini, anakuwa na furaha na hana mawazo. Hivyo anajikuta akisoma kwa utulivu darasani,” alisema.
Kwa upande wake, Stepen Kanyomoza, mzazi wa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kimuli, alisema shule hiyo imekuwa na mazingira mazuri ya malezi na elimu kwa wanafunzi.
Alisema walimu wamekuwa wakifuatilia changamoto zinazowakabili wanafunzi na kuwasaidia kuzitatua, jambo ambalo limekuwa likiwajengea mazingira mazuri ya kujifunza.
“Shuleni hapo hakuna ukatili kwa watoto,Walimu wanawafundisha na pia wanaangalia shida zao. Wanawasikiliza na kuwasaidia kadiri wanavyoweza mpaka mwanafunzi anafikia hatua nzuri,” alisema Kanyomoza.
Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, Frolah Kagaruki, alisema kwa kipindi cha miaka minne mfululizo, ufaulu wa wanafunzi katika shule za sekondari za Halmashauri hiyo umekuwa ukiongezeka.
Alisema shule hizo zimeendelea kupata wanafunzi wenye ufaulu wa Daraja la Kwanza hadi la Tatu, huku kukiwa hakuna aliyepata Daraja la Nne wala Sifuri, jambo alilolitaja kuwa ni ushindi mkubwa kwa Halmashauri hiyo.
Kagaruki alisema mafanikio hayo yametokana na bidii na ushirikiano kati ya walimu, Serikali na wadau wa elimu, wakiwemo wazazi na walezi.
Kwa takwimu za mwaka huu, alisema kati ya wanafunzi 746 waliofanya mtihani katika shule 13 za sekondari zenye Kidato cha Tano, wanafunzi 526 walipata Daraja la Kwanza, 194 Daraja la Pili na 23 Daraja la Tatu.pia kumekuwa na ongezeko la idadi ya watahiniwa bila kushuka kwa kiwango cha ufaulu.
“Mafanikio haya yanatokana na bidii na ushirikiano kati ya walimu, Serikali na wadau, wakiwemo wazazi na walezi. Tumekuwa na ongezeko la watahiniwa bila kushuka kwa ufaulu,” alisema Kagaruki.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, Jemsi John, alisema Halmashauri imejiwekea utaratibu wa kuwapongeza na kuwapa moyo walimu na shule zinazofanya vizuri katika mitihani ya Taifa.
Alisema hatua hiyo inalenga kuhamasisha walimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuboresha ufaulu wa wanafunzi.
John aliwasihi wazazi kuendelea kushirikiana na walimu na kusikiliza maelekezo yanayotolewa na shule, akisema walimu wamepewa dhamana na uwezo wa kuwaongoza wanafunzi katika kufikia malengo yao ya kielimu.
Mafanikio ya Shule ya Sekondari Kimuli yanaendelea kuonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya shule, wazazi, Serikali na jamii katika kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunza na kufanya vizuri kitaaluma.






Comments
Post a Comment