Na Mashaka Mhando, MWANZA
NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (maarufu kama Mwana FA au 'Falsafa'), ameacha historia mpya jijini Mwanza baada ya kufanya maajabu jukwaani akiungana na kundi lake la zamani la East Coast Team.
Tukio hilo la kukata na shoka limejiri usiku wa Agosti 8, 2026, katika ukumbi wa Climax uliopo Rock City Mall, wakati wa Tamasha kubwa la kusherehekea Miaka 30 ya muziki wa Bongo Fleva, ambapo Mhe. Mwinjuma alihudhuria kama Mgeni Rasmi.
Badala ya kuishia kutoa hotuba za kiserikali pekee, Mhe. Mwinjuma aliwapa mashabiki suprise ya kufa mtu alipopanda jukwaani na kuimba sambamba na wakali wenzake wa East Coast Team waliotikisa anga la muziki miaka ya nyuma, akiwemo Crazy GK, AY, na Snare.
Muunganiko huo wa East Coast Team jukwaani uliamsha shangwe za mashabiki na kukumbusha enzi za dhahabu za muziki huo, huku Mwana FA akidhihirisha kuwa makali yake ya kuchana mistari bado yako palepale licha ya kubeba majukumu mazito ya kiserikali.
Kuenzi Historia ya Bongo Fleva
Tamasha hilo linaloungwa mkono na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), limelenga kuwakutanisha wanamuziki wakongwe na wadau mbalimbali, likiwa ni sehemu maalum ya kuenzi historia, mchango, na safari ndefu ya muziki wa Bongo Fleva nchini Tanzania.
Mbali na kutoa burudani, tamasha hilo limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kukumbusha misingi madhubuti iliyojengwa na kizazi hicho cha waasisi, ambao walipambana kuweka ramani ya Bongo Fleva inayolipa mamilioni kwa wasanii wa kizazi cha sasa.







Comments
Post a Comment