NA: MWANDISHI WETU
Kodi ni chanzo muhimu cha mapato kinachoiwezesha serikali kufanikisha mipango na mikakati yake ya kimaendeleo kwa wananchi wake.
Wananchi wanahitaji huduma nzuri za kijamii kama elimu, afya, maji, umeme, barabara na masoko. Aidha, wanahitaji pia kuwezeshwa kiuchumi kwa kupatiwa mikopo nafuu ya kuwawezesha kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha shughuli za kibiashara na za kiujasiriamali.
Ni kwamba, mambo haya mazuri na mengine mengi, hayawezi kufanikiwa endapo serikali haitakuwa na fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wao. Hapa ndipo umuhimu wa ulipaji kodi unapoonekana.
Kimsingi, pamoja na umuhimu wa ulipaji kodi kwa maendeleo, walipakodi wanazo changamoto ambazo wanahitaji kuziwasilisha serikalini kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili ziweze kufanyiwa kazi.
Iko hivi: Ulipaji kodi unahusisha wadau wawili yaani TRA na walipakodi. Kutokana na hili, haitawezekana ulipaji kodi ukawa na ufanisi endapo walipakodi hawatatatuliwa changamoto zao kwa wakati.
Pia, kwa upande wa TRA, hawataweza kukusanya kodi kwa uendelevu mzuri ikiwa walipakodi wao wamesongwa na changamoto lukuki.
Ndiyo maana, kwa kutambua umuhimu wa pande zote kuwa na uhusiano mzuri na kufanikisha ulipaji kodi, TRA wameamua kuitenga siku ya Alhamisi ya kila wiki, nchi nzima, katika ofisi za wilaya na mikoa, kusikiliza kero za wafanyabiashara na walipakodi kwa ujumla.
Na hapa, Meneja Elimu Kwa Mlipakodi TRA, CPA Paul Walalaze, anasema, kutokana na umuhimu wa ulipaji kodi unaozingatia utu, siku ya Alhamisi imetengwa kwa upekee kabisa, kuhakikisha walipakodi wanawasilisha changamoto zao kwa uwazi ili kupata ufafanuzi na ufumbuzi wake.
"Hatuwezi kufanikiwa ukusanyaji kodi kama walipakodi wetu wamesongwa na changamoto. TRA imetenga siku hii ya Alhamisi, wafanyabiashara watoe changamoto zao, maoni na ushauri ili azma ya kukuza maendeleo nchini kwetu ifanikiwe," amesema.
Ameongeza kuwa, "Sasa, siku ya Alhamisi imekuwa jukwaa muhimu kwa walipakodi nchini. Ni siku ambayo walipakodi wanaonana na maofisa mapato kueleza changamoto zao, kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kikodi na kibiashara ili kuweza kufanya shughuli zao katika mazingira mazuri zaidi".
Ikumbukwe kuwa, mwelekeo wa serikali ni kujitegemea kibajeti kwa asilimia kubwa. Mwelekeo huu umejengwa katika misingi kuwa, nchi inajengwa na wananchi wenyewe.
Pamoja na ukweli kuwa, serikali haitaacha kupokea misaada kutoka kwa wadau na wabia wa maendeleo, lakini misaada hiyo itukute tukiwa katika safari yetu ya kujisimamia na kujitegemea kibajeti kufanikisha miradi ya maendeleo na ya kimkakati.
Ukweli ni kwamba, hatutaweza kufikia dhamira hii njema, endapo walipakodi hawatatatuliwa changamoto zao, ikizingatiwa kuwa walipakodi ndiyo waliobeba hatma ya maendeleo ya nchi kupitia ulipaji kodi.
Kwa kusisitiza hili, CPA Walalaze amesema, "Ewe mlipakodi mwenye changamoto, itumie siku ya Alhamisi kuwasilisha changamoto yako ili ipatiwe ufumbuzi. Utatuzi wa kero za kikodi utawezesha ulipaji kodi kufanyika vizuri na kujenga uhusiano mzuri baina ya Mamlaka na walipakodi wao".
Kwahiyo, mlipakodi hana sababu ya kulalamika, analo jukwaa rasmi la kuwasilisha changamoto zake kwa ufumbuzi zaidi. Utatuzi wa changamoto za walipakodi, utarahisisha ulipaji kodi wa hiari na kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Comments
Post a Comment