WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka nchi za Afrika na washirika wa kimataifa ziweke kipaumbele kwenye ajenda ya kutokomeza ugonjwa wa sotoka kwa mbuzi na kondoo (Peste des Petits Ruminants-PPR) kwa kuimarisha misaada ya kifedha na kiufundi.
“Mpango wa kutokomeza PPR si uwekezaji katika afya ya mifugo pekee, bali pia ni uwekezaji katika usalama wa chakula, kupunguza umaskini, kukuza biashara ya mifugo na kuimarisha ustahimilivu wa kiuchumi kwa wananchi. Tunatakiwa kuhakikisha ajenda hii inaendelea kupewa kipaumbele katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa ili kufikia lengo hili,” amesema.
Ametoa wito huo leo (Jumatatu, Septemba 21, 2026) wakati akitoa hotuba kuu kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa mkutano wa siku tatu wa Kimataifa wa Kujadili Afya Moja na Mifumo ya Chakula na Kilimo ulioanza leo katika Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), jijini Roma, Italia.
Akielezea mafanikio ya Tanzania katika kutokomeza ugonjwa wa sotoka, Waziri Mkuu amesema Serikali ililifanya suala hilo kuwa jambo kitaifa na inaendelea kutetea jitihada za kutokomeza ugonjwa huo barani Afrika.
“PPR si tu tatizo la afya ya wanyama. Kwa mamilioni ya kaya za wafugaji, hasa zile zinazotegemea kondoo na mbuzi, ni tishio kwa usalama wa chakula, mapato ya kaya, biashara na maisha,” amesema.
Katika mwaka wa fedha wa 2025/2026, Dkt. Mwigulu amesema Tanzania ilichanja kondoo na mbuzi milioni 16.8 dhidi ya sotoka na ilifanikiwa kufikia sehemu kubwa ya wanyama 17.2 waliolengwa kupata chanjo katika maeneo hatarishi.
“Kwa mwaka 2026/2027, zaidi ya sh. bilioni 30.8 (takriban dola milioni 11.6) zimetengwa kuendeleza awamu ya pili ya kampeni. Uzoefu wetu umetupa somo rahisi kwamba sotoka haiwezi kuondolewa kwa chanjo pekee bali kunahitajika jitihada zaidi. Inahitaji uchunguzi, utambuzi na ufuatiliaji wa wanyama, huduma sahihi kwa mifugo, ushirikiano baina ya nchi na nchi, na ufadhili endelevu.”
“Kuthibitisha hilo, Tanzania ilikuwa mwenyeji mkutano wa kikanda kuhusu masuala ya sotoka uliofanyika jijini Dar es Salaam tangu tarehe 14 hadi 16 Septemba 2026, na kuzikutanisha nchi saba kutoka Kusini, Kati na Mashariki mwa Afrika ili kuimarisha hatua za kudhibiti na kutokomezwa kwake.
Amesema mkutano huo ni matokeo ya mazungumzo ya awali ya kikanda, ikiwa ni pamoja na warsha ya sotoka iliyofanyika Arusha Aprili, 2026 ambayo ililenga kuwianisha mbinu zinazozingatia mfumo wa ikolojia katika ukanda wa Maziwa Makuu.
Waziri Mkuu amesema mada ya mkutano huo: “Afya Moja katika Mifumo ya Kilimo ni afya ya kila mtu, ni wajibu wa kila mmoja wetu, na inahitaji hatua za kila mmoja wetu,” inabainisha ukweli kwamba afya ya watu, wanyama, mimea na mifumo ya ikolojia haiwezi kutenganishwa.
“Kwa Tanzania, Afya Moja siyo tu ni dhana ya kisera bali ni wito wa kuchukua hatua. Inamaanisha kuwekeza katika mifumo inayozuia magonjwa kabla hayajawa majanga, kulinda chakula na maliasili zetu, kudumisha maisha na kuimarisha uthabiti wa jamii na uchumi wetu,” amesisitiza.
Awali, akiwakaribisha washiriki kwenye mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Bw. Qu Dongyu alisema Afya Moja huanzia shambani, ghalani, msituni, kwenye mito na bahari na popote pale ambapo wanyama, mimea, na watu hushiriki pamoja kuvuta hewa, kutumia udongo na maji. “Afya Moja huanzia pale maisha yanapounganishwa na hakuna mahali ambapo hilo linaonekana zaidi kuliko katika mifumo yetu ya chakula cha kilimo,” alisema.
Alisema udongo unapoharibiwa, mazao na malisho hudhoofika, mifumo ya ikolojia, watu na wanyama huwa hatarini zaidi, hivyo basi kuhatarisha lishe na maisha. Uduni wa maji hubeba vimelea vya magonjwa kati ya wanyama na watu, na hivyo kuongeza utegemezi wa dawa za kuua viini, jambo ambalo husababisha upinzani wa vimelea.
“Tunahitaji kufanya kazi kwa ukamilifu. Kinga na utayari ni muhimu - kuanzia mimea yenye afya, wanyama wenye afya nzuri, maji salama na udongo wenye afya. Miunganisho hiyo hiyo hupitia mazao yetu, misitu, uvuvi na bahari. Tunahitaji suluhu zilizounganishwa yaani Suluhu za Afya Moja,” amesisitiza.
Mapema, Rais wa Uswisi, Waziri Mkuu wa Serbia, Mawaziri wa Afya, Kilimo, Chakula na Mazingira kutoka Bangladesh, Ufaransa, Ireland, Tunisia na Jamhuri ya Korea walizungumza kwenye ufunguzi huo na kusisitiza kuwa utekelezaji wa dhana ya Afya Moja haupaswi kubaki kuwa jukumu la sekta ya afya pekee na badala yake, unahitaji ushiriki na uwajibikaji wa kila mdau yaani serikali, sekta binafsi, wakulima, wafugaji, watafiti, vijana, jamii za asili, asasi za kiraia, taasisi za fedha na wananchi kwa ujumla.










Comments
Post a Comment