Na Mwanamkuu Mwandoro, Tanga.
Umuhimu wa maandalizi na uwepo wa vifaa vya utafutaji na uokoaji umeonekana kupitia mazoezi yaliyofanyika wakati wa muendelezo wa shughuli zilizoandaliwa katika maadhimisho ya siku ya usafiri majini Duniani ambayo yamelenga kuhakikisha wahusika wanakuwa tayari kuchukua hatua pindi ajali au hatari inapotokea baharini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TASAC,Mussa Mandia katika zoezi la utayari lililofanyika raskazon swimming clab jijini Tanga Kwa lengo la kuonesha jamii kazi za uokoaji zinavyokuwa zikifanyika.
"Zoezi hili linaonyesha kwa vitendo thamani ya vifaa, kanuni na mipango ya utafutaji na uokoaji katika kuhakikisha watu wako tayari kuchukua hatua pale hatari inapotokea katika usafiri wa majini,” amesema Mandia
Katika zoezi hilo, nahodha alitoa amri kwa watu kuondoka kwenye chombo kilichokuwa katika hatari ya kupata ajali, huku timu ya uokoaji ya TASAC 1 ikifika na kuwasaidia watu waliokuwa kwenye chombo hicho.
Awali, Mwenyekiti wa Maadhimisho hayo taifa, Stella Katondo, amesema utafutaji na uokoaji ni sehemu muhimu ya usalama wa maisha ya binadamu katika usafiri wa majini.
Katondo ameongeza kuwa Tanzania imeingia katika mikataba mbalimbali ya kimataifa inayolenga kuhakikisha usalama wa binadamu unakuwa kipaumbele katika shughuli za usafiri wa majini.
Aidha zoezi la utafutaji na uokoaji lililopewa jina ‘Abandon the Ship’ lililenga kuonyesha hatua zinazopaswa kuchukuliwa wakati chombo kinapopatwa na maafa na abiria wanahitaji kuokolewa.
Alisema vifaa vinavyotumika katika uokoaji ni pamoja na jaketi za kuokoa maisha (life jackets), boti za kuokoa maisha (lifeboats) na maboya ya uokoaji (life rafts).
Maadhimisho hayo yameandaliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Shirika la Uwakala wa Meli Zanzibar (ZMA), kwa lengo la kuonyesha mchango wa usafiri wa majini katika biashara, ajira na maendeleo ya nchi, pamoja na kusisitiza umuhimu wa usalama wa maisha katika shughuli za usafiri wa majini.






Comments
Post a Comment