Na Mashaka Mhando, Tanga
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tanga, kimetangaza maandalizi kabambe ya mapokezi ya watu 1,000 kumlaki Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi, Mafunzo na Uenezi Taifa, Kenan Kihongosi, anayetarajiwa kufanya ziara ya siku mbili mkoani humo kuanzia Septemba 25.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Septemba 23, Kaimu Katibu wa Siasa na Uenezi Wilaya ya Tanga, Kipanga Salum Juma, alisema mapokezi hayo makubwa yatafanyika siku ya Ijumaa kuanzia saa nne asubuhi kwenye mzunguko wa njia panda ya Kwaminchi.
"Watu wa Jiji la Tanga zaidi ya 1,000 tutampokea kwa bashasha na vifijo pale kwenye Round About ya Kwaminchi. Tunafanya hivi kwa mapenzi makubwa kwa kuwa Ilani ya CCM imetutendea mema katika Jiji letu," alisema Kipanga.
Ratiba na Shughuli Kuu za Ziara
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, Kihongosi akipokelewa na mwenyeji wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC), Ustadh Rajab Abdurahman Abdallah, atahutubia mkutano mkubwa wa hadhara siku ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Lamore uliopo Kata ya Majengo. Katika mkutano huo, Kihongosi anatarajiwa kuzungumza na wananchi, kusikiliza, na kutatua kero zao mbalimbali ambazo watamuuliza.
Kabla ya kuhutubia mkutano huo wa hadhara, mwenezi huyo atakagua mradi mkubwa wa ujenzi na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Tanga. Kipanga alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imetoa fedha nyingi kuboresha uwanja huo ili uendane na kasi ya miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa mkoani humo.
Alitaja baadhi ya miradi hiyo ya kimkakati inayoenda sambamba na uboreshaji wa uwanja wa ndege kuwa ni pamoja na:
Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP)
Uboreshaji wa Bandari ya Tanga
Mradi mkubwa wa usafishaji mafuta (Refinery) unaotarajiwa kuanza wakati wowote.
Ziara Wilayani Mkinga na Miradi ya Ndani
Akifafanua zaidi kuhusu ratiba ya siku ya kwanza (Ijumaa), Kipanga alisema baada ya mapokezi na kikao na viongozi wa CCM Mkoa, Kihongosi ataelekea Wilayani Mkinga. Akiwa huko, atakagua ujenzi wa nyumba za watumishi wa CCM zinazojengwa katika wilaya zote tisa za kichama mkoani humo.
Nyumba hizo, ambazo ni za kwanza kwa chama hicho kujengwa katika ngazi ya mkoa nchi nzima, zinafadhiliwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Ustadh Rajab Abdallah, ambaye ametoa kiasi cha Shilingi bilioni 2.5 kuhakikisha zinakamilika. Kwa sasa, nyumba hizo zipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji.
Hii ni ziara ya kwanza kwa Kihongosi mkoani Tanga tangu achaguliwe kushika wadhifa huo mwaka jana, jambo linalofanya wakazi wa Tanga kuwa na shauku kubwa ya kumsikiliza na kuwasilisha matatizo yao moja kwa moja kwa uongozi wa juu wa chama hicho.
Hivyo, mwenezi wa wilaya amewaalika wakazi wa Jiji la Tanga na kutoka wilaya nyingine za mkoa wa Tanga, kujitokeza kwa wingi kumlaki mgeni huyo mkubwa katika chama na kumsikiliza kusikia namna serikali ilivyotekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2025-30.


Comments
Post a Comment