📍 Ataka maji yaanze kuingia kwenye tenki
Na Mashaka Mhando, Korogwe
WAZIRI wa Maji, Jumaa Awesso, amempa ultimatum ya siku tisa mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 Mkoani Tanga, kuhakikisha anafanya majaribio ya kusukuma maji na kuyaingiza kwenye tanki kuu kabla ya kuanza kusambazwa rasmi kwa wananchi.
Agizo hilo limetolewa leo Septemba 21 na Waziri Awesso mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo katika eneo la Tabora, Wilayani Korogwe, ambapo alimtaka mkandarasi huyo kukamilisha jaribio hilo kufikia tarehe 30 Septemba mwaka huu.
Waziri Awesso alieleza kuwa majaribio hayo ya kusafirisha maji kutoka kwenye chanzo kilichopo Mswaha yatasaidia kubaini na kutatua changamoto zote za kiufundi mapema, kabla ya mradi huo kukamilika kikamilifu mwezi Novemba na Desemba mwaka huu.
"Nimefarijika mradi huu ambao upo hatua za mwisho ili kuhakikisha mradi unaanza na kuwanufaisha wananchi, kwa hali niliyoiona namuelekeza mkandarasi leo tarehe 21 mwezi wa 9, nampa siku tisa mpaka tarehe 30 maji yatoke kule mtoni yaanze kuingia katika eneo hili la WTP (Water Treatment Plant) ili tuanze kutest kabla ya kuyaelekeza kwa wananchi," alisisitiza Waziri Awesso akiitaka kampuni ya JWIL Sustainable Water Management inayotekeleza mradi huo kuongeza kasi.
Akizungumzia utayari wa usambazaji, Mkurugenzi Mtendaji wa Mradi wa Maji wa HTM, Alawi Ahmed, alisema kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu maji yataanza kuingizwa kwenye mtandao rasmi, na wananchi walioomba kuunganishiwa huduma hiyo watapatiwa maji.
Mradi huo mkubwa unatarajiwa kuleta mapinduzi ya huduma ya maji mkoani humo, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba—akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian—alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa takribani Shilingi bilioni 170 kuufanikisha.
Kolimba alibainisha kuwa mradi huo utawanufaisha zaidi ya wakazi 870,000 katika wilaya nne za Korogwe, Handeni, Muheza na Pangani, na kwamba uongozi wa mkoa umeyapokea maelekezo ya Waziri ili kuhakikisha mkandarasi anaanza kusukuma maji mara moja.
Katika hatua nyingine, Waziri Awesso aliwataka watendaji wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha wanafikisha huduma ya maji katika vijiji 400 mwaka huu, na kutimiza lengo la kufikia vijiji vyote 1,575 vilivyosalia ifikapo mwaka 2030, ikizingatiwa kuwa hadi sasa vijiji 10,758 tayari vimefikiwa.
"Nawaomba watendaji wote wa Wizara ya Maji mkae mguu sawa. Fedha zipo za kutekeleza miradi ya maji vijijini ili kutimiza ndoto ya kumtua mama ndoo kichwani," alisema Awesso huku akiomba wadau wa maendeleo, benki na mashirika ya hiari kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.
Kuhusu tishio la mvua za El-Niño, Waziri aliziagiza Mamlaka za Mabonde na watendaji wa wizara hiyo kufanya ukaguzi wa mapema wa miundombinu ya maji na mabwawa ili kuzuia maafa, huku akiwataka kutumia mvua hizo kama fursa ya kuvuna maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kilimo cha umwagiliaji.









Comments
Post a Comment