NA: MWANDISHI WETU
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Taasisi ya Women and Youth Future Initiative (WYFI) wamepongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Kinara wa Nishati Safi Barani Afrika.
Pongezi hizo zimetolewa Agosti 7, 2026, Jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa Taasisi ya WYFI.
Taasisi ya WYFI inaongozwa na Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Asha Baraka, ambapo imejikita kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi kupitia fursa mbalimbali za maendeleo.
"Kutokana na jitihada alizoonyesha Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan katika kupigania matumizi ya nishati safi ya kupikia, tumeona tumpongeze na kumtia moyo kwa kazi kubwa na nzuri anazofanya," amesema Baraka.
Katika tukio hilo, Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia, Nolasco Mlay, alimwakilisha Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mlay aliwahimiza vijana na wanawake kutokuwa tegemezi wa ajira pekee, bali kutumia ubunifu, teknolojia na mitandao ya kijamii kujitengenezea fursa za kiuchumi.
Aidha, alieleza kuwa sekta za nishati safi, viwanda, kilimo, uvuvi na utalii zinaendelea kutoa nafasi nyingi za uwekezaji na ajira, hivyo ni muhimu kwa vijana kuendelea kujifunza na kujiongezea ujuzi ili kuzitumia kikamilifu.
Kwa upande wake, Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, CPA Paul Walalaze, alitoa elimu juu ya misamaha mbalimbali na nafuu za kikodi zinazotolewa na serikali ili kuchochea ukuaji wa biashara.
"Wafanyabiashara wadogo wakataosajiliwa na kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), watapata msamaha wa kodi ya mapato katika kipindi cha mwaka mmoja, ni vyema wakatumia fursa hii kuboresha biashara zao," amesema Walalaze.
Katika hatua nyingine, amefafanua misamaha ya Ongezeko la Thamani (VAT) inayotolewa kwenye bidhaa na huduma zinazohusiana na nishati safi.
Kwa mfano, vifaa vinavyotumika katika teknolojia za nishati mbadala ili nishati kama gesi na umeme vipatikane kwa bei nafuu, akitolea mfano smart meters za kusimamia matumizi ya nishati safi zimesamehewa VAT.
Sanjari na hilo, amehimiza wafanyabiashara, walipakodi na wananchi kwa ujumla, kuendelea na moyo wa uzalendo wa kulipa kodi kwa hiari ikizingatiwa kodi ndiyo nyenzo ya kufanikisha miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa kizazi cha sasa na kijacho.






Comments
Post a Comment