Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Mhe.Kambarage Masato Wasira, ametoa Kompyuta 10 za Kisasa kwa ajili ya kusaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza matumizi ya teknolojia katika shule zilizopo katika Kata 10 za Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Kompyuta hizo zimekabidhiwa kwa uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda kupitia mwakilishi wa Mbunge huyo, Elly Mwabe, ambaye ameeleza kuwa msaada huo ni sehemu ya mpango wa Mhe.Wasira wa kuendelea kushirikiana na jamii katika kuboresha elimu, hususan katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe.Aswege Kaminyoge amesema kompyuta hizo zitakabidhiwa kwa Halmashauri ya Mji wa Bunda ili wataalamu na viongozi wa halmashauri wabaini maeneo yenye uhitaji mkubwa na kuzisambaza kwa shule husika.
Amesema dunia ya sasa inahitaji wanafunzi kuwa na uelewa wa teknolojia, hivyo upatikanaji wa kompyuta mashuleni ni muhimu katika kuwaandaa wanafunzi kukabiliana na mahitaji ya elimu ya kisasa.
“Watoto wetu walioko mashuleni wanahitaji kompyuta bila kompyuta hawaendi sambamba na dunia ya sasa. Ninaamini vifaa hivi vitakuwa chachu ya kuongeza kiwango cha ufaulu katika Halmashauri ya Mji wa Bunda,” amesema Kaminyoge.
Mkuu huyo wa Wilaya pia amewataka wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha elimu, akisema milango iko wazi kwa mtu au taasisi yoyote yenye nia ya kuchangia maendeleo ya wananchi wa Bunda.
Amesisitiza kuwa vifaa hivyo vinapaswa kutunzwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili wananchi waweze kuona matokeo ya uwekezaji huo katika sekta ya elimu ambapo amemwekekeza Mkurugenzi wa Mji wa Bunda kuhakikisha vifaa hivyo vinawafikia walengwa.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mbunge wa Afrika Mashariki, Elly Mwabe, amesema Mhe.Wasira alishindwa kuhudhuria hafla hiyo kutokana na kuwa katika ziara ya kikazi ya Kamati ya Bunge la Afrika Mashariki Mjini Mogadishu, Somalia, lakini alitoa maelekezo ya kuwakilishwa na kukabidhi kompyuta hizo kwa Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Mwabe amesema mpango huo hautakuwa wa mara moja, bali Mhe.Wasira amedhamiria kuendelea kusaidia shule katika Halmashauri za Mkoa wa Mara kadiri atakavyokuwa na uwezo.
“Amesema mpango huu utakuwa endelevu. Kadiri atakavyokuwa akipata fedha, ataendelea na mpango huu ndani ya halmashauri zote za Mkoa wa Mara,” amesema Mwabe.
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Bunda Ndg.Gasper Petro Charles ameipongeza hatua hiyo na kusema Chama Cha Mapinduzi kimeupokea msaada huo kwa mikono miwili, huku akimfikishia Mhe.Wasira salamu za shukrani na kumtaka asiishie hapo kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo katika shule.
Gasper amesema Serikali imeendelea kujenga shule na madarasa kwa kasi, jambo ambalo limeongeza umuhimu wa upatikanaji wa vifaa vya TEHAMA ili wanafunzi waweze kupata elimu inayoendana na wakati.
Amesema wadau mbalimbali wanaendelea kujitokeza kuunga mkono juhudi hizo, akitolea mfano wa misaada mingine iliyotolewa katika Halmashauri ya Mji wa Bunda, ikiwemo mashine za photocopy zilizotolewa kwa shule.
“Mahitaji bado ni makubwa. Tunamwomba Mhe.Mbunge wa Afrika Mashariki aendelee kutusaidia na asisite, kwa sababu mchango wake una umuhimu mkubwa katika kuboresha elimu,” amesema Gasper.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Mhe.Minza Shani, amemshukuru Mhe.Wasira kwa kuamua kuanza na sekta ya elimu, akisema elimu ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii.
Shani amesema Halmashauri ya Mji wa Bunda ina changamoto mbalimbali katika sekta na idara zake, lakini hatua ya kuwekeza katika elimu ni muhimu kutokana na nafasi yake katika kuandaa kizazi cha sasa na kijacho.
Ameahidi kuwa kompyuta hizo zitasambazwa katika Kata zote 10 kwa kuzingatia maeneo yenye uhitaji mkubwa, bila upendeleo, huku wawakilishi wa wananchi wakishirikishwa katika kubaini shule zitakazonufaika.
Amesema halmashauri itahakikisha vifaa hivyo vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na vinatunzwa ili viweze kuwahudumia wanafunzi kwa muda mrefu.
Msaada huo unatajwa kuwa sehemu ya juhudi za wadau mbalimbali kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto za vifaa vya TEHAMA mashuleni na kuwawezesha wanafunzi wa Bunda kupata maarifa ya teknolojia yanayohitajika katika elimu ya kisasa.
Viongozi hao wameeleza kuwa matumizi ya kompyuta yanaweza pia kuwasaidia walimu katika maandalizi ya mitihani na kazi mbalimbali za kitaaluma, huku wanafunzi wakipata fursa ya kuzoea matumizi ya teknolojia mapema.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni chachu ya kuimarisha elimu katika Halmashauri ya Mji wa Bunda, huku wadau wengine wakihimizwa kuendelea kujitokeza kusaidia katika maeneo yenye uhitaji.









Comments
Post a Comment