Wananchi pamoja na madalali wa biashara ya ardhi nchini wamehimizwa kutumia huduma za Landmax Real Estate Company Limited ili kufanya miamala ya ardhi kwa usalama, kuondokana na utapeli na kupunguza migogoro inayotokana na biashara zisizo rasmi za ardhi.
Wito huo umetolewa na Mbunge wa Jimbo la Mbozi na Mkurugenzi wa Landmax Real Estate Company Limited, Onesmo Mnkondya, wakati wa uzinduzi wa ofisi za kampuni hiyo uliofanyika Juni 24, 2026 jijini Dodoma.
Mnkondya amesema Landmax imeanzishwa kwa dhamira ya kuleta mapinduzi katika sekta ya ardhi na mali isiyohamishika kwa kutoa huduma za kitaalamu, zinazozingatia sheria na zinazolenga kulinda maslahi ya wananchi na wawekezaji.
Amesema kupitia kampuni hiyo, wananchi watapata huduma za uuzaji na ununuzi wa ardhi na mali isiyohamishika, ushauri wa uwekezaji, usimamizi wa mali, urasimishaji wa nyaraka za ardhi, uendelezaji wa miradi, tafiti za soko pamoja na ushauri wa kitaalamu unaowezesha uwekezaji wenye tija.
"Tunawaalika wananchi na madalali wote wanaotaka kununua au kuuza ardhi kutumia huduma zetu ili kuhakikisha miamala yao inafanyika kwa uwazi, usalama na kwa kuzingatia sheria za nchi," amesema Mnkondya.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amezitaka Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma kuongeza kasi ya utoaji wa huduma kwa wawekezaji ili kuendana na kasi ya ukuaji wa sekta binafsi, akisisitiza kuwa urasimu usio wa lazima unarudisha nyuma jitihada za Serikali katika kuvutia uwekezaji.
Amesema sekta binafsi ni injini muhimu ya ukuaji wa uchumi, hivyo taasisi za umma zinapaswa kutoa huduma kwa wakati ili kuwezesha mazingira rafiki ya uwekezaji.
"Ukichelewesha sekta binafsi, unakuwa unadhoofisha mchango wake katika ujenzi wa Taifa. Ni wajibu wa Halmashauri na taasisi zote kuhakikisha wawekezaji wanapata huduma kwa ufanisi na kwa wakati," amesema Senyamule.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Clayton Chipando, amewataka wananchi kuwa makini wanapofanya miamala ya ardhi kwa kutumia kampuni zinazotambulika kisheria badala ya njia zisizo rasmi ambazo zimekuwa chanzo cha ongezeko la matukio ya utapeli.
Amesema uwepo wa Landmax utasaidia kurejesha imani ya wananchi katika sekta ya ardhi kwa kuhakikisha miamala yote inafanyika kwa weledi, uwazi na kwa kuzingatia sheria, hatua itakayochangia kulinda mali za wananchi na kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini.
Uzinduzi wa ofisi za Landmax Real Estate Company Limited unaashiria hatua mpya katika kuimarisha utoaji wa huduma za kitaalamu katika sekta ya ardhi na mali isiyohamishika, huku ukilenga kujenga mazingira salama ya uwekezaji na kupunguza migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiwakabili baadhi ya wananchi.






Comments
Post a Comment