Na Mashaka Mhando, TANGA
HATUA ya Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha miundombinu ya usafirishaji imepata msukumo mpya mkoani Tanga, kufuatia Shirika la Reli Tanzania (TRC) kupokea shehena ya vipande 17,006 vya reli na vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya takribani Dola za Marekani Milioni 56.
Kupatikana kwa vifaa hivyo ni sehemu ya mkakati wa kuboresha Reli ya Kaskazini inayounganisha Bandari ya Tanga na mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, hatua inayotarajiwa kuchochea biashara na kukuza uchumi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
Akizungumzia mapokezi hayo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, amelipongeza Shirika la TRC huku akibainisha kuwa uwekezaji huo unaenda sambamba na utekelezaji wa miradi ya Reli ya Kisasa (SGR) inayoendelea nchini.
"Serikali inaendelea kuwekeza kwa nguvu katika miundombinu ya reli. Maboresho haya ya Reli ya Kaskazini yanalenga kuongeza kasi ya treni na uwezo wa kubeba mizigo mizito, hivyo kuongeza ufanisi mkubwa wa usafirishaji wa mizigo na abiria kutoka Bandari yetu ya Tanga," alieleza Mhe. Balozi Batilda.
Bandari na TRC Wafunguka
Ujio wa vifaa hivyo umepokelewa kwa matumaini makubwa na mamlaka za kiutendaji. Meneja wa TRC Kanda ya Tanga, Christopher Kalisti, alifafanua kuwa reli hizo mpya zitachukua nafasi ya zile za zamani ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikisababisha vizuizi vya mwendo (speed restrictions).
"Kipande hiki kinachoboreshwa ni kiungo muhimu sana cha biashara kwa sababu kinaunganisha Reli ya Kaskazini (Tanga-Kilimanjaro-Arusha) na Reli ya Kati, hivyo ufanisi wa safari utaongezeka maradufu," alisema Kalisti.
Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Tanga, Salehe Mbega, alisema uboreshaji wa reli hiyo ni turufu muhimu kwa ushindani wa bandari hiyo kwani utaongeza kasi ya utoaji wa mizigo. Alibainisha kuwa sasa bandari itakuwa na uwezo mkubwa wa kuhudumia shehena zinazoelekea nchi za Afrika Mashariki, zikiwemo Rwanda na Burundi.
Ulinzi wa Miundombinu
Kutokana na ukubwa na thamani ya uwekezaji huo unaofanywa na Serikali, Mkuu wa Mkoa, Balozi Dkt. Batilda alihitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi wote kuwa walinzi wa kwanza wa miundombinu hiyo. Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kuripoti mara moja vitendo vyovyote vya uhujumu au wizi wa mali za umma.






Comments
Post a Comment