NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, amesema Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) inaendelea kuwa chachu ya mageuzi katika sekta ya kilimo kwa kuwawezesha wakulima, wafugaji na wadau wa mnyororo wa thamani kupata huduma za kifedha zinazoongeza uzalishaji na tija.
Mhe. Chande ameyasema hayo alipotembelea banda la TADB katika Maonesho ya 32 ya Wakulima (Nanenane) yanayoendelea jijini Dodoma, ambapo alijionea huduma na programu mbalimbali zinazotekelezwa na benki hiyo kwa lengo la kukuza kilimo chenye tija na biashara.
Baada ya kupokea maelezo kutoka kwa wataalamu wa TADB, Naibu Waziri ameeleza kuridhishwa na namna benki hiyo inavyotekeleza dhamira yake ya kuwafikia wadau wa sekta ya kilimo kupitia mikopo na huduma nyingine za kifedha zinazowawezesha kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao na kipato.
Amesema hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa yenye tija, inaimarisha usalama wa chakula, inafungua fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
"TADB ina nafasi muhimu katika kuwezesha maendeleo ya kilimo nchini. Huduma zake zinaendelea kuwagusa wakulima, wafugaji na wajasiriamali wa kilimo, jambo linaloleta matokeo chanya katika uzalishaji na maendeleo ya wananchi," amesema Mhe. Chande.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na kuziunga mkono taasisi zinazowekeza katika maendeleo ya sekta ya kilimo, akisisitiza kuwa sekta hiyo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania na msingi wa maendeleo ya wananchi wengi.
Katika maonesho hayo, TADB inaendelea kutoa elimu kuhusu huduma zake, ikiwemo mikopo kwa wakulima, wafugaji, wavuvi, wasindikaji wa mazao na wawekezaji wa sekta ya kilimo, pamoja na programu maalum za kuwawezesha vijana, wanawake na wajasiriamali ili kuongeza ushiriki wao katika uchumi wa kilimo.





Comments
Post a Comment