MWAKIOJA: UWEKEZAJI WA ZAIDI YA BILIONI 82 KATIKA MAJI WAIPELEKA MKINGA KWENYE LENGO LA ASILIMIA 100
Mbunge wa Jimbo la Mkinga, Mhe. Twaha Said Mwakioja, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya maji wilayani Mkinga, hatua inayoweka msingi wa kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Akizungumza mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Mhe. Mwakioja amesema wananchi wa Mkinga wana kila sababu ya kuendelea kumpongeza, kumuombea na kumuunga mkono Rais Samia kwa namna ambavyo ameendelea kuelekeza rasilimali nyingi katika miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Amesema kwa sasa upatikanaji wa maji safi na salama wilayani Mkinga umefikia asilimia 72.6, huku vijiji 67 kati ya 75 vikipata huduma hiyo. Alibainisha kuwa vijiji vinane vilivyosalia vitaunganishwa na huduma hiyo kupitia miradi ya maji yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 47 inayoendelea kutekelezwa.
Mbunge huyo amesema, pamoja na miradi hiyo, Serikali imeidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 35 kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji utakaohudumia vijiji vyote vya Tarafa ya Mkinga. Alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika kabla ya Desemba mwaka huu na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kutoka asilimia 72.6 hadi asilimia 85.
"Tunaendelea kushirikiana na Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na viongozi wote kuhakikisha tunafikia lengo la kitaifa la upatikanaji wa maji safi na salama kwa asilimia 100 ifikapo mwaka ujao. Tuna imani kubwa kuwa kwa kasi ya utekelezaji wa miradi hii, ndoto hiyo itatimia," amesema Mhe. Mwakioja.
Aidha, amewataka wananchi kuwa walinzi wa kwanza wa miradi ya maji inayotekelezwa na Serikali kwa kuitunza na kuilinda dhidi ya uharibifu, akieleza kuwa uwekezaji huo wa zaidi ya shilingi bilioni 82 una thamani kubwa kwa maendeleo ya Mkinga na ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya miradi hiyo hayatategemea Serikali pekee, bali pia ushiriki wa wananchi katika kuitunza miundombinu hiyo ili huduma ya maji iendelee kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Wilaya ya Mkinga.




Comments
Post a Comment