* Ampongeza Aweso kwa kuandaa timu 80, ashangaa kuizidi Ligi Kuu.
*Na Mashaka Mhando, Pangani
NAIBU Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma maarufu 'MwanaFA', amekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mashindano makubwa ya soka ya 'Aweso Cup' yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Sakura, wilayani Pangani.
Akizindua mashindano hayo kwa kupiga penalti ya kifundi, MwanaFA alimmwagia sifa Mbunge wa Pangani ambaye pia ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kwa kuwekeza kwenye michezo na kufanikiwa kukusanya timu takribani 80 kutoka kata 14 za jimbo hilo.
"Hongera Mheshimiwa, timu 80 siyo mchezo! Umeishinda hata Ligi Kuu yetu yenye timu 16 tu. Hili ulilolifanya si jambo dogo," alisema MwanaFA kwa mshangao.
MwanaFA alibainisha kuwa Serikali imeweka mpango madhubuti wa kuhakikisha kila yanapofanyika mashindano ya mpira wa miguu, haijalishi yana udogo gani, inapeleka skauti kutoka Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kusaka vipaji ili kuvilea kama inavyofanya kwa timu za vijana chini ya miaka 17.
Alisisitiza kuwa kutokana na ukubwa na muda mrefu wa mashindano ya Aweso Cup, watahakikisha skauti wa TFF wanafika Pangani kuvumbua vipaji. Pia, aligusia maandalizi ya AFCON 2027, akieleza kuwa Serikali inajenga viwanja vipya Arusha na Fumba (Zanzibar), kukarabati Uwanja wa Amani na Benjamin Mkapa, pamoja na kujenga viwanja 15 vipya vya mazoezi.
Kwa upande wake, Msemaji wa Timu za Taifa, Haji Manara, alimpongeza Mhe. Aweso huku akichomekea utani kuwa katika mechi ya ufunguzi ameona washambuliaji wazuri kuliko Ousmane Doumbia aliyewahi kusajiliwa na klabu ya Simba.
"Mheshimiwa hongera sana kwa uwekezaji huu. Nimeona wachezaji na washambuliaji wazuri hapa kuliko Doumbia wa Simba," alitania Manara na kuongeza siri kuwa Pangani iliwahi kutoa mchezaji bora wa Ligi Kuu nchini, Fadhil Bwanga (aliyechezea Yanga), hivyo Aweso Cup itumike kumsaka 'Bwanga mwingine'.
Katika hatua nyingine, Katibu wa CCM Wilaya ya Pangani, Abdul Swala, alikoshwa na kasi ya maendeleo ya Mhe. Aweso na kutamka kuwa wananchi wameridhika naye kiasi cha kutaka aendelee kuwa mbunge hadi mwaka 2050.
"Mheshimiwa sisi hatuna tabu na wewe, kazi unazozifanya ni kubwa na tunaridhika. 2030 wewe ndiye mbunge, 2035 ni wewe, 2040 ni wewe, 2045 pia ni wewe, 2050 huko sasa utapambana na hali yako," alisema Swala huku akishangiliwa na umati uliokuwa uwanjani.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo (DAS), Esther Gama, alisema mashindano hayo yatachezwa kwa mfumo wa mtoano (Knock-out) na kutaja zawadi nono zinazowasubiri washindi:
* Mshindi wa Kwanza (Bingwa):Tsh Milioni 10
* Mshindi wa Pili: Tsh Milioni 5
* Mshindi wa Tatu: Tsh Milioni 3
* Kikundi Bora cha Ushangiliaji: Pikipiki aina ya Boxer.
Akihitimisha hafla hiyo, Waziri Jumaa Aweso alisema lengo kuu la mashindano hayo ni kuibua vipaji na kuvitengenezea njia ya ajira, akiwataka vijana kutumia fursa hiyo kufika mbali kitaifa na kimataifa.
Pia, Aweso alitumia wasaa huo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kufungua miradi ya barabara, afya, na elimu inayoifanya Pangani kung'ara.
"Mkakati wetu ni 'kuitoa Pangani pangoni' na kuiweka kwenye ramani kama zilivyo wilaya nyingine bora hapa nchini. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuunga mkono katika miradi mbalimbali ya kijamii," alihitimisha Aweso.










Comments
Post a Comment