Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imetangaza matokeo ya Mitihani ya Kati Awamu ya Pili ya Taaluma ya Mnyororo wa Ugavi, ambapo watahiniwa 275 kati ya 528 waliofanya mitihani hiyo wamefaulu, sawa na asilimia 52.1.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Sept 18,2026 Jijini Dodoma wakati wa kutangaza matokeo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya wataalamu WA ununuzi na Ugavi (PSPTB), Godfred Mbanyi, amesema jumla ya watahiniwa 567 walidahiliwa kufanya mitihani hiyo iliyofanyika kuanzia Agosti 30 hadi Septemba 4, 2026.
"Kati yao, watahiniwa 528 walifanya mitihani, huku 39 wakishindwa kufanya kwa sababu mbalimbali". Amesema
Mbanyi amesema watahiniwa 232, sawa na asilimia 43.9, wamepata nafasi ya kurudia baadhi ya masomo (referral), huku 21, sawa na asilimia 4.1, wakifeli na hivyo kulazimika kuanza upya masomo yao katika ngazi husika.
"Tunawapongeza watahiniwa waliofaulu katika ngazi mbalimbali, wakiwemo waliokidhi sifa za kutunukiwa vyeti vya Professional Diploma, Graduate Professional na CPSP". Amewapongeza
Mbanyi pia amewapongeza wahadhiri na wakufunzi kutoka vyuo na vituo mbalimbali vya mafunzo kwa mchango wao katika kuwaandaa watahiniwa na kuwawezesha kufanya vizuri katika mitihani hiyo.
Amesema watahiniwa waliofaulu Professional Diploma (I & II), Graduate Professional (I, II & III) pamoja na Research wamealikwa kushiriki katika Mahafali ya 15 ya PSPTB.
Kwa wale ambao hawakufanya vizuri, Mbanyi amewataka kujisajili na kufanya mitihani ya awamu inayofuata itakayofanyika Novemba 9 hadi 13, 2026, huku akieleza kuwa usajili umefunguliwa kuanzia Septemba 8 hadi Oktoba 24, 2026.
Aidha, amewataka watahiniwa wenye hali ya referral ya “last chance” kutumia fursa hiyo katika mitihani ya Novemba 2026 kukamilisha ngazi zao, kwa kuwa baada ya mitihani hiyo hali hiyo itaondolewa kwa mujibu wa mtaala wa Bodi.
Mbanyi amewakaribisha pia wahitimu wa vyuo vikuu nchini na nje ya nchi kujisajili na kufanya mitihani ya kitaaluma ya PSPTB ili kupata sifa stahiki katika taaluma ya Ununuzi na Ugavi.
Vilevile, amewataka wazazi, wadhamini na waajiri kuwawezesha watahiniwa kwa kulipia ada za maandalizi na mitihani, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza wataalamu wenye maarifa na ujuzi katika sekta ya Ununuzi na Ugavi.
Katika hatua nyingine, PSPTB imewataka watahiniwa kuzingatia kanuni na taratibu za mitihani na kujiepusha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili, ikisisitiza kuwa haitasita kuchukua hatua dhidi ya watakaobainika kukiuka taratibu hizo.
Kwa mujibu wa kanuni za Bodi, hatua hizo zinaweza kujumuisha kufutiwa matokeo ya mitihani, kusimamishwa kufanya mitihani kwa vipindi vitatu, kulipa faini au kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kifungo.


Comments
Post a Comment