NA GHATI MSAMBA, Musoma.
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Fadhil Maganya, ameiomba Serikali kuendelea na mchakato wa marekebisho ya Katiba, akisema wananchi na vyama mbalimbali bado wanahitaji Katiba Mpya.
Maganya alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mara.
Alisema Serikali haipaswi kusikiliza sauti za watu wanaopinga mchakato huo bila kutoa mawazo chanya, akisisitiza kuwa mchakato wa Katiba Mpya unapaswa kuendelea kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025.
“Serikali iendelee na mchakato wa Katiba Mpya kwa sababu wapo wananchi na vyama vingine vinavyohitaji Katiba Mpya. Ni chama kimoja pekee ambacho hakihitaji,” alisema.
Alisema suala la Katiba linahitaji utulivu, busara na maridhiano, hivyo kuwataka wanaharakati na wanasiasa kuepuka kutumia nguvu kubwa katika kushinikiza madai yao.
Maganya alisema katika kipindi cha takribani wiki mbili kumekuwa na mijadala katika majukwaa mbalimbali kuhusu upatikanaji wa haraka wa Katiba Mpya, huku baadhi ya wadau wakitaka mchakato huo uharakishwe.
Alisisitiza kuwa maridhiano katika suala hilo si jambo la Serikali na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pekee, bali ni jambo linalowahusu Watanzania wote.
“Ninavyoona, tunachelewa kupata Katiba Mpya kutokana na mikanganyiko inayojitokeza,” alisema.
Aidha, Maganya alitoa mfano wa mchakato wa Katiba uliofanyika mwaka 1984, akisema ulihusisha matumizi makubwa ya fedha na rasilimali.
Alisema ni muhimu kwa wadau wote kujifunza kutokana na historia hiyo na kuhakikisha mchakato wa sasa unafanyika kwa utulivu na kwa kuzingatia maslahi ya Watanzania.
Pia aliwataka wanachama na viongozi wa CHADEMA kuwa na busara na kuepuka kuingia katika migogoro, akiwakumbusha kile alichodai kuwa kilitokea mwaka 2025.
Maganya alisema tofauti za kisiasa zinapaswa kushughulikiwa kwa njia za mazungumzo, maridhiano na kutumia njia za kikatiba badala ya nguvu.





Comments
Post a Comment